Na,Jumbe Ismailly IKUNGI
HALMASHAURI ya wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida imepokea zaidi ya shilingi milioni 700 kutoka serikali kuu na kutenga shilingi milioni 50 kwenye bajeti yake kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma kwa lengo la kupunguza vifo vya akina mama na watoto wilayani hapa.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi,Miraji Jumanne Mtaturu aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo,uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Ikungi.
Aidha Mtaturu alifafanua kwamba kati ya kiasi hicho cha fedha,shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Kituo ch afya Ihanja na shilingi milioni 220 zitakazofanikisha upatikanaji wa vitendeakazi pamoja na vifaa tiba.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya huyo vifaa vitakavyonunuliwa ni pamoja na vifaa vya fyeta,vifaa vya maabara,kuboresha chumba cha kuhifadhia maiti ili iwe na uwezo wa kuhifadhi takribani maiti sita kwa wakati mmoja na huduma za mama na mtoto vikiwemo vitanda vyake.
“Tumeshapata fedha shilingi milioni mia tano na tayari zipo site kuboresha huduma za afya wenye Kituo cha afya Ihanja tayari kazi kubwa inapofanyika pale na kwa kupitia hili kwa kweli,tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais,Dk.John Pombe Magufuli kwa kufanya kazi znuri ya kutuletea fedha zile”alisisitiza huku akishangiliwa na madiwani.
“Lakini pia kuleta shilingi milioni 220 ambazo tumeshazipeleka tayari MSD kwa ajili ya kununua vifaa,vifaa vya fyeta,vifaa vya maabara,chumba cha kuhifadhia maiti tutaweka yenye uwezo wa kubeba takribani maiti sita kwa wakati mmoja,tutakuwa na huduma ya mama na mtoto,vitanda vyake kila kitu na kama nilivyosema kwamba fyeta itakayokuwepo pale itasaidia upasuaji ambao ulikuwa hauna sababu kupeleka sehemu nyingine.”aliweka bayana mkuu huyo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya huyo tayari Halmashauri hiyo imetenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuboresha kituo cha afya cha Ikungi zitakazosaidia kutengeneza chumba cha upasuaji.
Hata hivyo Mtaturu ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama wa wilaya ya Ikungi alibainisha pia kuwa fedha hizo zimetumika kujenga nyumba ya mganga,kuweka miundombinu ya maji ya mvua kusaidia kuondoa tatizo la maji kwenye eneo hilo.
Mkuu huyo wa wilaya aliweka bayana pia kwamba lengo la millennia ni kupunguza na hiyo ni dhamira ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk.John Pombe Magufuli ni kuhakikisha inapunguza vifo vya mama na mtoto.
Akisoma taarifa ya mapato na matumizi,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Abeli Richard alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa kukusanya mapato ni kutokana na kushuka kwa mapato yatokanayo na ushuru wa mazao kutokana na kupungua kwa mazao na tozo za ushuru kwa mazao ya chakula kutoka asilimia tano hadi asilimia mbili.
Hata hivyo Makamu mwenyekiti huyo aliitaja mikakati yao kuwa ni kutoa maelekezo kwenye kamati za maendeleo za kata ili ziweze kujadili suala la mapato ya Halmashauri kwa kila kikao na kusimamia utekelezaji wa maazimio yanayohusiana na ukusanyaji wa mapato.
Akifunga mkutano huo wa kawaida wa Baraza la madiwani,Mwenyekiti wa Halmashauri,Ally Nkhangaa alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anatayarisha kwa uhakika zaidi fedha za madeni ya posho za madiwani hao ambao kwa takribani miezi miwili bado hawajalipwa stahili zao.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni