WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba kuhakikisha inadhibiti ongezeko la mimba kwa watoto wa shule.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 28, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba.
Waziri Mkuu amesema ni lazima viongozi hao wasimamie nidhamu kwa kuwalinda watoto wa kike katika wilaya hiyo wasipate mimba ili waendelee na masomo.
“Kwa nini kila mwaka mimba Tandahimba zinaongezeka, viongozi simamieni utekelezaji wa sheria kwa kuwachukua hatua wote waliowapa mimba wanafunzi.”
Amesema lazima wahusika wote wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwa sababu wanaharibu elimu ya motto wa kike jambo ambalo si zuri.
Waziri Mkuu ametolea mfano mwaka 2015 wafunzi 10 walipata mimba, mwaka 2016 waliopata mimba walikuwa 20, mwaka 2018 waliongeza na kufikia 57.
Amesema takwimu hizo haziridhishi, hatua kali zichukuliwe kudhibiti vitendo hivyo na Serikali haitaki kusikia mwanafunzi ameacha shule kwa sababu ya kupata mimba.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na wafuate sheria.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi amewasisitiza watumishi wa umma wawafuate wananchi vijijini na wawahudumie ipasavyo.
Amesema Rais Dkt. John Magufuli amesisitiza watumishi wa umma wawatumikie wananchi bila ya ubaguzi wowote pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
“Serikali inataka kila mtumishi atimize wajibu wake na haina muda wa kuwalea watumishi wazembe, wala rushwa na wasiowajibika, hivyo watambue wajibu wao.”
Pia amewataka Madiwani wa Halmashauri hiyo wahakikishe wanakwenda kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 28, 2018.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni