Mwanariadha Usain Bolt anatarajiwa
kucheza katika kikosi cha wachezaji 11 wa dunia dhidi ya wachezaji 11
wa Uingereza watakaoongozwa na Robbie Williams katika mechi ya
kuchangisha fedha itakayochezwa kwenye dimba la Old Trafford, Juni 10
mwaka huu.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa
mwanariadha huyo aliyestaafu mbio kucheza soka katika dimba la klabu
anayoipenda ya Manchester United, huku mshindi huyo wa medali nane za
dhahabu katika Olimpiki akitarajiwa kuwa kivutio miongoni mwa nyota
wa mchezo huo.
Orodha ya vikosi hivyo vya mchezo
huo wa kuchangisha fedha ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
la Kuwahudumia Watoto- UNICEF, vitahusisha nyota wa soka na mastaa wa
tasnia za burudani utachezwa siku nne kabla ya kuanza michuano ya
kombe la dunia Urusi.
Nyota huyo Mjamaica Bolt mwenye umri
wa miaka 31, jana aliibua uvumi kwa watu wanaomfuatilia kwenye
mitandao ya jamii baada ya kuandika kuwa ametia saini kuchezea klabu
ya soka, na watu kuhisi kuwa amejiunga na Manchester United.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni