Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala (aliyeshika kifimbo), akikagua alama ya mpaka kati ya Pori la Akiba Mkungunero na Kijiji cha Ikengwa, wilayani Kondoa mkoani Dodoma. Nyuma aliyevaa ushungi ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Ikengwa, Nade Laida, akibubujikwa machozi wakati wa mkutano kati ya wanakijiji na msafara wa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mwanamke huyo ni mmoja wa waathirika wa mgogoro baina ya Pori la Akiba Mkungunero na wananchi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo.
Wakazi waishio jirani na Pori la Akiba la Mkungunero lililoko Wilayani Kondoa mkoani Dodoma, wameiomba Serikali iwarejeshee eneo la kilometa 12 kuanzia kwenye vijiji vyao kwenda ndani ya Pori hilo ambalo wanadai limechukuliwa kinyemela na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuathiri maisha yao yanayotegemea kwa kiasi kikubwa kilimo na ufugaji.
Wakazi wa vijiji vya Ikengwa, Keikei Tangini, Keikei na Kisondoko, wametoa maombi hayo mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala wakati alipofanyaziara katika vijiji hivyo vinavyozunguka Pori hilo la Akiba ili kutatua mgogoro wa muda mrefu baina ya Pori hilo na wananchi wanaolizunguka.
Wananchi na viongozi wa vijiji hivyo wameeleza kuwa uwekaji wa mipaka ya Pori hilo haukuwa shirikishi na kwamba maeneo makubwa ya vijiji yaliyokuwa yakitumiwa na wananchi kwa shughuli zao za kilimo, ufugaji na makazi yametwaliwa na kusababisha mgogoro huo.
Malalamiko mengine ya wananchi hao ni kunyanyaswa na watumishi wa Pori la Akiba Mkungunero kwa kupigwa, kunyang'anywa mifugo yao, na baadhi yao kudai kuumizwa na baadhi ya wenzao kuuawa kwa risasi na askari wanaolinda Pori hilo.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji, ameiomba Serikali kutumia busara na kurejesha eneo lililochukuliwa kimakosa kutoka kwa wananchi ili waweze kujiendeleza kiuchumi na kuishi kwa amani na utulivu.
"Najua wewe ni mwadilifu ndio maana umeaminiwa na Mhe. Rais, najua utawatendea haki wananchi wa vijiji hivi ili nao wajione ni wananchi halali katika Taifa lao huru la Tanzania tukienda hatua kwa hatua bila kuvunja sheria za nchi" alisisitiza Dkt. Kijaji
Amefafanua kuwa maeneo yaliyochukuliwa na Pori hilo yalikuwa yakitumiwa na wananchi kwa muda mrefu na kwamba mchakato wa kupandisha hadhi eneo hilo kutoka Pori Tengefu hadi kuwa Pori la Akiba la Mkungunero haukuwashirikisha wananchi.
Akijibu Hoja za Wananchi hao, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi kwa ustawi na maendeleo ya nchi, aliwahakikishia wananchi hao kwamba Serikali itatafuta njia ya bora ya kuumaliza mgogoro huo kwa maslahi ya pande zote mbili, wananchi na Serikali.
"Ni lazima tutafute mahali ambapo tutabalance, maslahi ya umma na maslahi mapana ya Taifa zima na niwahakikishie kuwa tutafanyakazi hiyo kwa uadilifu, uzalendo mkubwa, lakini zaidi kwa kuzingatia maslahi yenu wananchi wenzetu" Alisisitiza Dkt. Kigwangala.
Awali, Meneja wa Pori hilo, Emmanuel Birasso, alieleza kuwa mchakato wa kuanzisha Pori hilo la Akiba Mkungunero ulifuata taratibu za kisheria za uanzishwaji wa mapori ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi jambo ambalo linapingwa na wananchi hao.
Alieleza kuwa mpaka sasa takriban kilometa 118 za mpaka wote wa Pori umesimikwa alama za mipaka na kuwaondoa watu wanaodaiwa kuvamia Pori hilo pamoja na kuimarisha ulinzi na doria.
Pori Tengefu la Mkungunero (Game Controlled Area) lilipandishwa hadhi na kuwa Pori la Akiba la Mkungunero mnamo mwaka 1996 kwa Tangazo la Serikali (GN) namba 307, likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 743.95.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni