WAKULIMA wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani wa Pwani wamefurahia kupokea mbegu bora ya mahindi aina ya Wema 2109 kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa na Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa ajili ya kupandwa kwenye mashamba darasa katika halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mbegu hiyo kwenye uzinduzi wa mashamba darasa katika vijiji vya Diozile na Kibindu vilivyopo Kata ya Msoga mkoani humo Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Pwani,Kapilima George alisema mbegu hiyo itasaidia kuongeza tija ya uzalishaji wa mahindi katika halmshauri hiyo hivyo amewataka wakulima kuichangamkia.
"Tuwashukuru COSTECH na OFAB kwa kutuletea mbegu hii ambayo kwetu itakuwa ni mkombozi mkubwa katika mkoa wetu hasa kwa wakulima wa Kata ya Kibindu ambao ni vinara kwa kilimo cha mahindi katika mkoa wetu" alisema George.
Alisema mkoa wa Pwani kwa mwaka jana ulizalisha tani 110 za mahindi huku tani 65 zikizalishwa na Kata ya Kibindu jambo la kuwapongeza wakulima wa kata hiyo.Alisema mbegu hiyo itaongeza msukumo wa kilimo ilimo cha mahindi kwenye halmashauri hiyo hivyo kujikwamua kupata baa la njaa na ziada kuuza.
Aliwaomba wakulima hasa kwa wanavikundi waliopata mbegu hizo kuhakikisha wanayatunza mashamba darasa hayo kwa manufaa ya wakulima wote wa wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH wakati wa kukabidhi mbegu hizo, Mkurugenzi wa Fedha wa Fedha na Utawala wa COSTECH, Shabani Hussein alisema .kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kilimo na kuhakikisha zinawafikia walengwa ambao ni wakulima.
Alisema mbegu hizo walizozikabidhi zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa hazina ubora.
Matifiti Kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro, Mikidadi Hamidu alisema iwapo mkulima atafuata ushauri wa upandaji wa mbegu hiyo ya Wema 2109 katika ekari moja atapata magunia 35 tofauti na mbegu nyingine ambapo wanapata chini ya hapo.
Aliongeza kuwa mbegu hiyo italeta matokeo mazuri iwapo kanuni za kilimo bora zitafuatwa kama vile kufuata vipimo, maandalizi ya shamba, matumizi ya mbolea zote ya kupandia na kukuzia na kuwa mbegu hiyo ni moja kati ya mbegu 11 zilizofanyiwa utafiti.
Ofisa mradi huo kutoka COSTECH, Bestina Daniel alisema kwa mkoa huo wametoa mbegu kilo 58 kwa ajili ya mashamba darasa katika wilaya ya Bagamoyo na Chalinze ambapo kwa wakulima mmoja mmoja wametoa kilo 42 pamoja na mbolea ya kupandia.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni