Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) inatarajiwa kuchezwa mwishoni mwa mwezi Machi katika viwanja vinne tofauti nchini.
Ijumaa Machi 30, 2018 kutakuwa na mchezo mmoja katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, ambapo wenyeji Stand United watawakaribisha Njombe Mji saa 10:00 jioni.
Machi 31, 2018 kutakuwa na michezo miwili, Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku saa 2:00 usiku Azam FC watakua wenyeji wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Jumapili Aprili Mosi, 2018 kutakuwa na mchezo mmoja, Singida United watakuwa wenyeji wa Young Africans katika uwanja wa Namfua mjini Singida Aprili Mosi, 2018 mchezo utakaonza saa 10:00 jioni.
TSHITSHIMBI MCHEZAJI BORA MWEZI FEBRUARI
Kiungo wa timu ya Yanga, Papy Tshishimbi Kabamba amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Februari 2018.
Tshishimbi ametwaa nafasi hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili alioingia nao katika kinyang’anyiro kwa mwezi Februari, katika uchambuzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo iliyokutana Dar es Salaam wiki hii.
Kiungo huyo alitoa mchango mkubwa ulioiwezesha Yanga kupata pointi 12 katika michezo minne iliyocheza, ikiwa ndiyo timu pekee kwa mwezi huo kushinda michezo yote.
Katika michezo hiyo, Tshishimbi aliibuka mchezaji bora katika michezo mitatu, ambapo pia kwa mwezi huo alifunga mabao matatu na kutoa pasi ya mwisho moja iliyozaa bao.
Walioshindana na Tshishimbi ni Pius Buswita wa Yanga, ambaye pia alichangia mafanikio hayo ya Yanga kwa mwezi huo, huku pia akifunga mabao mawili.
Mwingine aliyeingia hatua ya fainali ni Emmanuel Okwi wa Simba aliyeisaidia timu yake kupata pointi 10 kwa michezo minne, ikishinda mitatu na kutoka sare mmoja, huku Okwi akifunga mabao manne.
Buswita naTshishimbi hawakupata kadi yoyote, wakati Okwi alipata kadi moja ya njano.
Kwa ushindi huo,Tshishimbi atazawadiwa fedha taslimu sh.1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc, Pia atazawadiwa kisimbuzi (decoder) kutoka kwa wadhamini wa matangazo wa Ligi hiyo Azam TV pamoja na ngao ya kumbukumbu ya ushindi wake.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni