Taifa Stars inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki katika kalenda ya FIFA inayoanza Machi 19 – 27, 2018 dhidi ya timu za Taifa za Algeria na DR Congo.
Stars itasafiri kuelekea jijini Algiers kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji Algeria Machi 22, 2018 na baada ya mchezo huo dhidi ya Algeria, Taifa Stars itarejea nyumbani kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Congo DR Machi 27, 208 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
TWIGA STARS YAINGIA KAMBINI
Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imeingia kambini katika Hostel za Makao Makuu ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT Mlalakuwa) kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake AFCON 2018 nchini Ghana.
Twiga Stars itacheza dhidi ya Zambia (She Polopolo) Aprili 4, 2018 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na marudiano kufanyika April 8, 2018 jijini Lusaka nchini Zambia.
Mshindi wa jumla kwa raundi hii atacheza na mshindi kati ya Namibia v Zimbabwe mwezi Mei, na atakayeibuka mshindi atafuzu moja kwa moja kwa Fainali hizo za Wanawake Afrika.
NGORONGORO HEROES KUCHEZA NA MOROCCO NA MSUMBIJI
Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Morocco na Msumbuji kabla ya kuwavaa DR Congo katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Vijana (AFCON U20).
Ngorogoro Heroes itacheza na timu ya Taifa ya Vijana ya Morocco Jumamosi Machi 17, 2018 na dhidi ya timu ya Taifa ya Vijana Msumbiji Jumatano Machi 21, 2018 michezo yote ikichezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON U20, Ngorogoro Heroes itacheza dhidi ya DR Congo Machi 31 katika uwanja wa Taifa na mchezo wa marudiano kufanyika baada ya wiki mbili jijini Kinshansha Congo DR.
Ngorongoro Heroes imeingia kambini katika Hoteli ya Ndege Beach iliyopo Mbweni ambapo inajiandaa na michezo hiyo miwili ya kirafiki na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Vijana Afrika wenye umri chini ya miaka 20.
SERENGETI BOYS KAMBINI KUJIWINDA NA CECAFA
Timu ya Taifa chini ya miaka 16 Serengeti Boys inaendelea kujiandaa na mashindano ya CECAFA kwa vijana yatakayofanyika Burundi.
Kikosi hicho kipo kambini kwenye hostel za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF,Karume-Ilala,Dar es Salaam.
Mashindano hayo ya CECAFA kwa Vijana yataanza April 1 mpaka April 15 huko Burundi.
U-13 KWENDA UBELIGIJI
Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U13) inatarajiwa kushiriki michuano ya vijana itakayozikutanisha timu za vijana za nchi zaidi ya 10 kutoka mataifa mbalimbali yatakayofanyika nchini Ubelgiji mwezi Agosti, 2018.
TFF inaandaa utaratibu sahihi wa kupata kikosi cha timu ya Taifa kwa vijana wenye umri huo ili kuweza kujiandaa na michuano hiyo ya vijana.
Kwa kuanzia kutachezwa mechi kati ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 kutoka Tanzania Bara dhidi ya vijana wa Zanzibar katika siku za hivi karibuni ili kutoa nafasi kwa waalimu kuchaguwa wachezaji wenye vipaji watakaounda kikosi hicho cha U13.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni