Release No. 207
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 8, 2013
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa
uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusukuma mbele
zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini.
Ametoa
changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga na
kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila utakapohitajika katika
shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.
Rais
Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa
ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye binafsi
(Rais Kikwete) na Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza
mpira wa miguu nchini.
“Pongezi
zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha kiwango
cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
“Kwa
niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwako wewe
na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu muhimu mlioutoa wa kuendeleza
mpira wa miguu nchini.
“Mafanikio
ya kutia moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika
barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli zake.
Hata
hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo inapataka, lakini
dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni uongozi mpya
kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu nchini.
Tenga
ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika
Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba
2004 hadi Oktoba 2013.
PAMBANO LA
TANZANITE LAINGIZA MIL 5/-
Pambano
kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya
Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini (Basetsana) lililochezwa jana
(Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 5,353,000.
Washabiki
waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Dunia, Kanda
ya Afrika iliyomalizika kwa The Tanzanite kulala mabao 4-1 walikuwa 4,282.
Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.
Mgawo
wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh.
816,559.32, gharama za kuchapa tiketi sh. 1,649,754, asilimia 20 ya gharama za
mchezo sh. 577,573) wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 433,003.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata sh. 144,334.33 huku Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh. 1,732,012.01.
Mechi
iliyopita ya Tanzanite dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Oktoba 26 mwaka huu Uwanja
wa Taifa, na timu hiyo kushinda mabao 10-0 ilishuhudiwa na watazamaji 5,003 na
kuingiza sh. 6,190,000.
Tanzanite
na Basetsana zitarudiana kati ya Desemba 20 na 22 mwaka huu jijini
Johannesburg, Afrika Kusini.
MECHI YA KILIMANJARO STARS KUPIGWA MACHAKOS
Mechi ya kwanza ya nusu fainali ya
michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji kati ya Tanzania Bara (Kilimanjaro
Stars) na wenyeji Kenya (Harambee Stars) itapigwa Uwanja wa Machakos.
Kwa mujibu wa ofisa wa CECAFA, Amir
Hassan mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Machakos ulioko takribani kilometa 64
kutoka jijini Nairobi. Mechi hiyo itachezwa Jumanne (Desemba 10 mwaka huu)
kuanzia saa 10 kamili jioni na itaoneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport
kupitia chaneli ya SS9.
Kilimanjaro Stars imetinga hatua hiyo
baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa mikwaju 3-2 ya penalti katika
mechi ya robo fainali ya michuano hiyo iliyochezwa jana Uwanja wa Aga Khan
katika Jiji la Mombasa.
Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika
timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Mabao ya Kilimanjaro Stars yalifungwa
na Mrisho Ngasa wakati katika mikwaju ya penalti walofumania nyavu ni Amri
Kiemba, Athuman Idd na nahodha Kelvin Yondani.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni