WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka
Watanzania waendelee kuombea amani ya Taifa zima bila kujali tofauti zao za dini
na kusisitiza kwamba kila mmoja ana wajibu wa kutunza amani iliyopo.
Ametoa wito huo jana jioni (Jumamosi, Desemba 7, 2013) wakati
akizindua Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania (Southern Tanzania Union Mission) la
Kanisa la Waadventista Wasabato kwenye sherehe zilizofanyika kwenye Viwanja vya
Mwalimu J. K. Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waumini zaidi ya 13,000
wa Kanisa hilo walioshiriki uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema: “Mtu asiyejua
vurugu hawezi kujua thamani ya amani... lakini lazima tujue madhara ya vurugu
huwa ni makubwa kwa watoto, wanawake na wazee.”
Aliwasihi viongozi wa kanisa hilo
pamoja na waumini kuendelea kuliombea Taifa pamoja na Watanzania wote. “Mimi
huwa nafarijika sana ninaposikia sehemu fulani kuna maombi kwa ajili ya Taifa,
kwa hiyo ninawaomba Maaskofu na waumini msichoke kuliombea Taifa letu,”
alisema.
Mbali na kuliombea Taifa pamoja na kuwaombea
waumuni wake, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa kanisa kuendelea kushirikiana
na Serikali kutafuta njia ya kuwasaidia waumini wake kukua kiuchumi. “Kanisa
lina wajibu wa kuwasaidia wananchi kukua kiuchumi na mimi natambua waumini wa
kanisa hili ni wakulima na wafugaji ama vyote viwili.”
Waziri Mkuu alisema moja ya kazi
kubwa ya kanisa ni kusaidia waumini wake kukua kiroho na kimwili. Lakini kanisa
pia linahitaji kuona maisha ya waumini yanakuwa bora zaidi. ”Tunategemea uchumi
wa muumini mmoja mmoja kukua na hivyo uchumi wa kanisa, na uchumi wa Taifa kwa
ujumla kukua,” alisongeza.
Alisema anataraji kwamba kupatikana
kwa Jimbo Kuu la Kusini kutakuwa ni chachu ya kupata maendeleo zaidi ya kiuchumi
katika Jimbo hilo ambalo linafaa sana kwa kilimo. “Pia, tunategemea kasi ya
kupata waumini wapya itaongezeka kutokana na kugawanywa kwa Jimbo Kuu moja na
kuwa Majimbo Makuu mawili, hivyo kusogeza huduma za kiroho na kiuchumi karibu
zaidi na waumini,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Jimbo Kuu la Kusini
lililozinduliwa jana linajumuisha mikoa ambayo ni maarufu kwa shughuli za
kiuchumi. “Imetajwa mikoa takriban 11 ya Tanzania Bara na Mitano ya Visiwani. Ipo
mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Lindi na Mbeya. Mikoa mingine
ni Morogoro, Mtwara, Pwani, Rukwa na Ruvuma. Hakika ni eneo kubwa la kuongoza.”
“Kinachotakiwa ni kwa Kanisa
kujipanga vizuri kwa kujiwekea mikakati ya maendeleo. Nawaombeni sana kuanzia sasa,
tuwahimize waumini wetu hasa vijana wajikite pia katika kuanzisha miradi ya
kilimo na ufugaji, ikiwemo kilimo cha mazao na ufugaji nyuki. Mkitumia fursa
hizi zinazowazunguka katika maeneo yetu ya Jimbo hili, mnaweza kabisa kuleta
ukombozi wa kiuchumi, hususan kwa vijana wetu,” alisisitiza.
Kanisa hilo lenye waumini wapatao
milioni 17.2 duniani, lina makao yake makuu nchini Marekani. Hapa Tanzania lina
waumini milioni tano na lilikuwa na jimbo kuu moja ambalo liligawanywa katika
majimbo sita na makao yake makuu kwenye mabano kama ifuatavyo:- Kaskazini
Mashariki (Same), Kusini mwa Ziwa Victoria (Mwanza), Mara (Musoma), Mashariki
(Morogoro), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Magharibi (Kigoma).
Mapema, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa
Jimbo Kuu la Kusini, Mchungaji James Machage alisema kutokana na kupanuka kwa
kazi, kanisa hilo limeona vema hapa nchini kuwe na majimbo makuu mawili badala
ya moja.
Alisema Jimbo Kuu la Kaskazini
ambalo makao yake makuu yatakuwa Arusha litahusisha majimbo ya Mara, Kusini mwa
Ziwa Victoria, Magharibi na Kaskazini Mashariki wakati Jimbo Kuu la Kusini
litahusisha majimbo ya Mashariki na Nyanda za Juu Kusini na makao yake makuu
yatakuwa jijini Dar es Salaam.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, DESEMBA 8, 2013
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni