Meneja Mawasiliano wa TANAPA Pascal Shelutete akizungumza na wanahabari jijini Arusha alipokuwa akitangaza Wanahabari waliofika fainali ya TUZO ZA HABARI ZA TANAPA ZA MWAKA 2013 wanaotarajiwa kukabidhiwa tuzo zao wiki ijayo jijini Mwanza wakati wa Mkutano wa kila mwaka wa TANAPA na Wahariri wa Habari nchini.
Jumla ya Waandishi wa Habari 10 wamefanikiwa kufikia hatua ya fainali ya Tuzo za Uandishi wa Habari za Shirika la Hifadhi za Taifa za mwaka 2013.
Wanahabari waliofanikiwa kufika hatua ya fainali ni pamoja na Frank Leonard (Habari Leo), Jackson Kalindimya (Nipashe), Humphrey Mgonja (Radio SAUT FM), Raymond Nyamwihula (Star TV) na Vedasto Msungu (ITV).
Wengine ni pamoja na Kakuru Msimu (Star TV), Gerald Kitabu (The Guardian), Salome Kitomari (Nipashe), David Rwenyagira (Radio 5) na Cassius Mdami (Channel Ten).
Hafla ya utoaji Tuzo za Habari za TANAPA itafanyika siku ya Jumanne tarehe 27 Mei, 2014 jijini Mwanza ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu.
Hafla hii itaenda pamoja na Mkutano wa kila mwaka baina ya TANAPA na Wahariri wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini inayotarajiwa kuanza wiki ijayo jijini Mwanza.
Jumla ya kazi zilizotumwa kwa ajili ya kushindanishwa mwaka huu ni 114 tofauti na kazi 34 za mwaka jana.
Ongezeko hili la asilimia 235 lililazimu Jopo la Majaji kutumia muda mwingi zaidi wa kupitia kazi zote na kupata washindi. Kati ya kazi 114 zilizotumwa, kazi zilizohusu Uhifadhi ni 64 (sawa na 56%) na kazi zilizohusu Utalii wa
Ndani zilikuwa 50 (sawa na 44%). Tuzo za Uandishi wa Habari za TANAPA hutolewa kila mwaka kwa nia ya kuwashirikisha wanahabari kushindanisha umahiri wa kazi zao katika kuelimisha jamii umuhimu wa dhana ya Uhifadhi kwa maeneo yaliyotengwa kisheria kama Hifadhi za Taifa na uhamasishaji wa Utalii wa Ndani kwa faida ya uchumi wa nchi yetu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni