Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (kushoto) akimsikiliza
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Maendeleo (UNDP) Bw. Philippe Poinsot alipomtembelea Naibu Waziri
ofisini kwake, Mtaa wa Mkwepu, jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu,
Mei 19, 2014). Kulia ni Naibu wake anayeshughulikia Programu Bi.
Mandisa Mashologu. (Picha na Wizara ya katiba na Sheria).
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki akiagana na Naibu Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo
(UNDP) Bi. Mandisa Mashologu (kulia) alipomtembelea Naibu Waziri
ofisini kwake, Mtaa wa Mkwepu, jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu,
Mei 19, 2014). Katikati ni Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Philippe
Poinsot.
Na Mwandishi Wetu
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) inatarajia kutoa
mafunzo kwa Waandishi wa Sheria kwa lengo la kuwaongezea uwezo wa
kuandaa miswada katika lugha ya kiswahili – lugha ambayo inatumiwa
na watanzania wengi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Angellah Jasmine Kairuki amemwambia Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw.
Philippe Poinsot kuwa kwa sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
inatekeleza mkakati wa kuandaa miswada yote inayosilishwa Bungeni
katika lugha mbili, Kiingereza na Kiswahili ili kuwawezesha wananchi
wengi kuisoma.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Naibu Waziri
Kairuki, katika kutekeleza kazi hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kupitia Idara ya Uandishi wa Sheria inakabiliwa na
changamoto kadhaa zikiwemo uhaba wa watumishi na uwezo na hivyo
kuhitaji msaada wa mafunzo.
“Kwa sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
ina kazi ya kuandaa miswada katika lugha mbili ikiwemo Kiswahili
ambayo ndiyo lugha ya taifa ambayo wananchi wengi wanaifahamu,”
alisema Bi. Kairuki katika mkutano wake na Bw. Poinsot leo (Jumatatu,
Mei 19, 2014) jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya
Naibu Waziri Kairuki jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju, Mkurugenzi wa
Mashtaka Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP
Bi. Mandisa Mashologu na maafisa wengine waandamizi wa serikali.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw.
Masaju alisema kwa sasa Ofisi yake ina Waandishi wa Sheria 18 tu na
kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na majukumu ya Idara ya
Uandishi wa Sheria.
“Serikali imeanzisha utaratibu huu wa
kuandaa miswada katika lugha mbili lakini tuna changamoto ya uhaba wa
watumishi na hata hao waliopo, walifundishwa kuandaa miswada katika
lugha ya kiingereza na hivyo kuhitaji mafunzo,” alisema Bw. Masaju.
Akiongea katika mkutano huo, Bw.
Poinsot alisema Shirika lake limepokea maombi ya Serikali na kuwa
litayafanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali ili hatimaye miradi
hiyo itekelezwe.
“Kwetu sisi UNDP, sekta ya sheria ni
muhimu sana hususan katika miradi inayolenga kuwasaidia masikini na
kujenga uwezo … ndiyo maana tupo tayari kuisadia,” alisema
kiongozi huyo wa UNDP hapa nchini.
Kwa mujibu wa Bw. Poinsot, Shirika lake
limepanga kuisaidia Serikali kupitia mradi wake unaolenga kuimarisha
usimamizi wa utoaji haki (Strengthening Administartion of Justice
Project). Miradi ya awali inatarajiwa kuanza kutekelezewa hivi
karibuni kabla ya kuanza kutekelezwa kwa awamu ya pili ya Mpango
Maalum wa Shirika hilo (UNDAP II) unaotarajia kuanza kutekelezwa
mwezi Januari 2015.
Maeneo mengine ambayo Serikali na UNDP
zinatarajia kushirikiana ni katika utoaji wa huduma za msaada wa
kisheria; kuimarisha uwezo wa waendesha mashtaka na watumishi wa
mahakama; na kuboresha mifumo ya uendeshaji ili kupunguza mlundikano
wa kesi mahakamani.
Mwisho.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni