Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhiwa Fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B “ Bibi Subira Mohammed kuomba ridhaa kwa CCM kugombea Uwakilishi Jimbo Jipya la Mahonda.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi {CCM} Wilaya ya Kaskazini “B “ Bibi Subira Mohammed akimpatia maelezo Balozi Seif mara baada ya kumkabidhi Fomu kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kugombea Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Jimbo la Mahonda hapo Ofisi ya CCM Wilaya hiyo Mahonda.
Balozi Seif akimkabidhi shilingi Laki 300,000/- Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Subira Mohammed ikiwa ni ada ya Fomu alizopewa kwa ajili ya kuomba kuteuliwa kugombea Uwakilishi Jimbo la Mahonda kwa Tiketi ya CCM katika uchaguzi Mkuu ujao.
Picha na –OMPR – ZNZ.
Wakati Chama cha Mapinduzi kimeanza zoezi la kutoa fomu kwa ajili ya Wanachama wake wenye nia kutaka kugombea nafasi za Uwakilishi, Ubunge, Udiwani na Viti Maalum vya wanawake, wazazi na Vijana mapema leo asubuhi baadhi ya wanachama wa chama hicho tayari wameshajitokeza kuchukuwa fomu hizo.
Zoezi hilo limekuwa likiendeshwa kwenye Ofisi zote za Chama cha Mapinduzi za Wilaya hapa Nchini na linatarajiwa kuendelea hadi Saa Nane Mchana ya Tarehe 19 mwezi huu wa Julai.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali ni miongoni mwa Wanachama hao wa CCM waliojitokeza kuchukuwa fomu hizo akijiandaa kuomba kuwania nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Jimbo Jipya la Mahonda ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Balozi Seif Ali Iddi ni Mmoja miongoni mwa Wanachama wanane wa CCM waliojitokeza hadi hivi sasa wenye nia ya kutaka kugombea nafasi ya Uwakilishi katika Majimbo mbali mbali ya Wilaya ya Kaskazini “B”ambao tayari wameshachukuwa Fomu hizo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Subira Mohammed akimkabidhi Fomu hizo hapo Ofisini kwake Mahonda alimueleza Balozi Seif kwamba yuko huru kujeresha fomu hizo wakati wowote amalizapo kujaza kuanzia leo hadi Tarehe 19 Julai majira ya Mchana.
Bibi Subira alisema Mwanachama mwenye nia ya kutaka kugombea nafasi hizo anawajibika kuzilipia Fomu hizo kwa kiwango cha shilingi Laki 300,000/- kama ada rasmi iliyowekwa na Chama pamoja na mwanachama huyo kuchangia chama kwa kadri ya kiwango anachokimudu.
Hadi sasa tayari wanachama wa Chama cha Mapinduzi wapatao kumi wameshajitokeza kuchukua Fomu za kuomba kugombea nafasi za Ubunge na Wanachama Wanne kwa Nafasi za Udiwani Ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Katika safari hiyo ya uchukuaji Fomu za kutaka kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba Mwaka huu wa 2015 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliambatana na wake zake wote wawili Mama Pili Seif Iddi na Mama Asha Suleiman Iddi na kushuhudiwa na baadhi ya Viongozi wa CCM Wilaya na Jimbo la Kitope.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni