.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 17 Julai 2015

DK. SHEIN AIPONGEZA INDIA KWA KUIUNGA MKONO ZANZIBAR KATIKA KUIMARISHA SEKTA ZA MAENDELEO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe,Debnath Shaw alipofikaIkulu Mjini Zanzibar leo,kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi Nchini, [Picha na Ikulu.]


                                                                            Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa hatua za India za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo zinadhihirishwa uhusiano mwema na wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati mazungumzo kati yake na Balozi wa India katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaemaliza muda wake wa kazi hapa nchini Mhe. Debnath Shaw yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliipongeza Serikali ya India kwa hatua yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo.

Dk.Shein alisema kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na India ambao umeanzishwa na waasisi wa nchi hizo akiwemo marehemu Julius Kambarage Nyerere na waasisi wa nchi hiyo akiwemo marehemu Indira Gandhi.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano kati yake na India hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwepo ushirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, biashara, viwanda na nyenginezo.


Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa India kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wake katika kuanzisha Chuo cha amali katika kijiji cha Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja ambacho wakati wowote kitazinduliwa.

Utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa Chuo hicho ulidhihirishwa wakati wa ziara ya Dk. Shein nchini India mnamo Febuari mwaka 2014 alipotembelea chuo cha ‘Barefoot” kilichoko katika Jimbo la Jajasthan nchini India.

Katika mazungumzo na Balozi huyo, Dk. Shein alieleza kuwa kukamilika kwa chuo hicho kutasaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa mafunzo ya amali na ujasiriamali sambamba na usambazaji wa umemejua na maeneo mengineyo ambapo mkazo mkubwa ni kuwawezesha wanawake wa vijijini kujikwamua na umasikini.


Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya India kwa nia yake ya kuendelea kutoa ushirikiano wake na kuunga mkono miradi ya maji, elimu na mengineyo huku akipongeza hatua zinazoendelea za kutekeleza makubaliano yaliofika katika ziara yake nchini.

Nae Balozi wa India katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Debnath Shaw alipongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na kuadi kuuendeleza kwa lengo la manufaa kwa pande mbili hizo.

Balozi Shaw alisema kuwa India itahakikisha inakamilisha miradi yote ya maendeleo ilioanzishwa kwa mashirikiano kati yake na Zanzibar kwa kutambua kuwa kukamilika kwa miradi hiyo ndio chachu ya kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano uliopo.

Aidha, Balozi Shaw alisema kuwa ziara ya Dk. Shein nchini India imeweza kupata mafanikio makubwa na kusisitiza imani yake kuwa makubaliano yote yaliofanyika baina ya India na Zanzibar yatatekelezwa kwa lengo la mafanikio kwa pande zote mbili. 

                                                                                                  Kwa hisani ya ZanziNews

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni