Halmashauri Kuu ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) leo imetangaza majina ya wagombea ubunge, ubunge
viti maalum, uwakilishi na uwakilishi viti maalum ambapo baadhi ya
wagombea walioshinda kwenye kura za maoni wametupwa nje na
kuchukuliwa mshindi wa tatu.
Akizungumza leo na waandishi wa
habari kwenye ofisi za makao makuu ya CCM mjini Dodoma, Katibu wa
Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema kuwa kuna baadhi ya majimbo
ambayo yamelazimika kurudia kupiga kura za maoni na mengine kuhesabu
upya kura zilizopigwa baada ya kujitokeza malalamiko kwa wagombea.
Amesema kuna baadhi ya majimbo
ambayo wamelazimika kumchukua mshindi wa tatu kwenye kura za maoni na
kuwaacha walioshinda nafasi ya kwanza na ya pili ili kumaliza
migogoro iliyokuwepo.
Ameyataja majimbo 11 ambayo
yatarudia uchaguzi wa kura za maoni kuwa ni Ukonga, Kiteto, Chilonwa,
Kilolo, Njombe Kusini, Makete, Namtumbo, Rufiji, Mbinga Vijijini,
Busega na Singida Mashariki.
Aidha Nnauye amesema kuwa uchaguzi
wa viti maalum kupitia umoja wa wanawake Tanzania (UWT) yamepitishwa
kama yalivyotoka mikoani ambapo ni mkoa mmoja tu wa Dar es Salaam
ambao NEC imetengua ushindi wa mshindi wa kwanza, Angela Kiziga
ambaye ni mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na badala yake
aliyeshika nafasi ya pili na ya tatu ndiyo waliopitishwa katika
ubunge wa viti maalum.
Waliopitishwa na Halmashauri Kuu ya
CCM kwenye ubunge wa viti maalum mkoa wa Dar es Salaam ni Mariam
Kisangi aliyekuwa mshindi wa pili na Janeth Masaburi aliyekuwa
mshindi wa tatu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni