MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) imegawa nyumba nyingine 16 kwa wanachama wake waliokamilisha ujenzi ambako mpaka sasa wanachama 120 wamekabidhiwa nyumba zao katika kijiji cha Wasanii cha Mwanzega, Mkuranga.
Katika hafla ya kukabidhi nyumba hizo jana, Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema mpango wa ujenzi wa nyumba hizo ni endelevu mpaka hapo ekari 300 zilizotengwa kwa ujenzi zitajengwa nyumba kwa mpango wa kuchangiana.
Taalib alisema aina za nyumba zinazojengwa kwa sasa ni za matofali ya saruji ya chuma kimoja kwa sh. 750,000, nyumba za vyumba viwili na sebule kwa sh. 3.8 na nyumba kubwa ya sh. mil. 6.4.
Alisema kipa wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa, Hamisi Kinye anatarajia kukabidhiwa nyumba yake Desemba mwaka huu sambamba na wasanii wengine Lilian Ndelwa, Edson Mwela, Happyness Magere, Asheri Kazeba, Jaqueline Joseph na Suzan Moshi ambao wamebadilisha nyumba walizokuwa wakabidhiwe za udongo na sasa watachukua nyumba zilizojengwa kwa saruji.
Mwenyekiti Taalib alisema SHIWATA imeandaa mpango mkakati wa kuingiza umeme na maji katika kijiji hicho kabla ya Desemba na tayari kikundi cha wasanii kimepiga kambi ya kujiandaa kurekodi tamthilia ya maisha ya Bongo katika kijiji hicho.
Mmoja wa wasanii aliyekabidhiwa nyumba ya sh. mil. 6.4, Mwajuma Kisengo alisema ametimiza ndoto yake ya kushirikiana na wasanii wenzake kuishi katika kijiji cha Mwanzega, Mkuranga.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni