Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Mbogo Futakamba akitoa zawadi kwa mfanyakazi bora wa mwaka 2015 toka DAWASCO wakati alipotembelea Shirika hilo mapema wiki hii. Pamoja na mambo mengine alielekeza shirika juu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Serikali ya kuunganisha Wateja Milioni Moja ifikapo June 2016. Picha na Everlasting Lyaro- DAWASCO.
WIZARA ya maji na umwagiliaji, imesema inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mipango ya usambazaji wa huduma za maji, inayofanywa na shirika la majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) na kutoa rai kwa watumishi wa shirika hilo kushirikiana ili kufikia malengo ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yalisemwa jana na katibu mkuu wa wizara hiyo mhandisi Mbogo Futakamba, alipokuwa akiwahutubia wafanyakazi wa DAWASCO, katika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Futakamba, alisema kasi ya utoaji wa huduma bora za maji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, imepunguza malalamiko mengi ya wananchi, na kwamba serikali imeanza kupata matumaini makubwa na kujenga imani kwa shirika hilo kwa kufanikisha malengo makuu ya usambazaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Aidha alisema kwa kiwango kikubwa wizara ya maji na umwagiliaji kwa sasa inajivunia kwa kazi nzuri iliyofanywa na shirika hilo, hasa kwa kuzingatia kuwa DAWASCO ndio jicho la wizara kutokana na wingi wa wananchi wanaohitaji huduma za maji zinazosambazwa na shirika hilo.
“Nimeona jitihada zenu, nimependa jinsi mnavyofanya kazi kama timu, naomba muwe na uaminifu mkubwa sana katika kazi, kuweni wawajibikaji ili wananchi wapate huduma ya maji”, alisema mhandisi Futakamba.
Katika hatua nyingine katibu mkuu huyo alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na shirika hilo za kupunguza kiwango cha upotevu wa maji pamoja na kudhibiti wizi wa maji, ambavyo vimekuwa kikwazo kinachochochea malalamiko ya wananchi kwa shirika hilo.
Awali akitoa taarifa ya shirika hilo, afisa mtendaji mkuu wa DAWASCO, mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema shirika hilo limefanikiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji, baada ya kuongeza uzalishaji kutoka mita za ujazo 7,834,234 hadi mita za ujazo 8,421,370 kati ya mwezi Mei hadi Novemba 2015.
Alizitaja sababu za mafanikio ya ongezeko la kiwango cha maji ni pamoja na udhibiti wa upotevu wa maji katika bomba kubwa, kufanya matengenezo ya tahadhari, maboresho ya maslahi ya wafanyakazi na kuboreshwa kwa kitengo cha upotevu wa maji.
Mhandisi Luhemeja alibainisha kuwa DAWASCO, imefanikiwa kufunga dira katika maungio ya maji, kuziba maeneo yanayovujisha maji kwa wakati, kupambana na wezi wa maji, kuhakiki ufanisi wa dira za maji, kusajili maboza ya wauzaji maji na kuboresha usomaji wa dira, ambavyo viliwezesha kupunguza kiwango cha maji yanayopotea kutoka asilimia 62 hadi 45, kati ya mwezi Mei mpaka Novemba 2015.
Aliongeza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya uboreshaji wa huduma za maji yaliwezesha shirika hilo la DAWASCO, kuongeza makusanyo ya mapato kutoka shilingi bilioni 2.9 hadi kufikia bilioni 6.2 kati ya mwezi Mei hadi Novemba 2015.
Wakati huo huo shirika hilo limeanza kutekeleza agizo la serikali linaloitaka DAWASCO, kuongeza idadi ya wateja wake hadi kufikia milioni moja, katika jiji la Dar es Salaam, miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani, hadi kufikia mwezi Juni 2016.
Katika utekelezaji wa agizo hilo DAWASCO iko katika utekelezaji wa Maagizo ya serikali ya kuhakikisha wananchi waishio katika Jiji la Dar s salaam, Miji ya Kibaha na Bagamoyo Mkoani Pwani wanaunganishiwa Maji ifikapo Julai 2016. Katika kutekeleza agizo hilo Dawasco imejipanga katika awamu kuu NNE (4)
1. Awamu ya kwanza itawahusu wateja wote walioko katika maeneo ambayo kwa sasa yanapata maji na kuna miundo mbinu ya mabomba karibu.
2. Awamu ya Pili itahusu maeneo ambayo yamepitiwa na mabomba makubwa ya Maji jirani lakini wananchi wake hawana maji kwa sababu ya kukosekana kwa miundo mbinu ya usambazaji.
3. Awamu ya Tatu itahusisha maeneo yote yaliyopitiwa na mradi maarufu wa Mabomba ya Kichina, Maunganisho katika awamu hii yataanza baada ya kukamilika kwa Miradi ya Ruvu Chini na Ruvu Juu,
4. Awamu ya Nne itaanza katika maeneo yote ambayo kwa sasa hakuna miundo mbinu ya Maji na yako mbali kutoka katika mabomba makubwa
Gharama ya kuunganishiwa huduma ya Majisafi ni Tsh 200,000 kwa wateja wadogo (Domestic Customers)na Tsh 400,000 kwa wateja wakubwa (Corporate Customers)
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni