Michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mzunguko wa tatu inatarajiwa kuendelea Januari 12 na wikiendi ya Januari 23-27 kwa timu 32 kuchuana kuwania kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.
Timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimeingia moja kwa moja mzunguko wa tatu ambapo sasa zinajumuika na timu 16 zilizofuzu kutoka raundi ya pili yenye timu kutoka ligi daraja la kwanza na ligi daraja la pili.
Jumamosi, Januari 12, Majimaji itacheza dhidi ya JKT Mlale uwanja wa Majimaji mjini Songea, Januari 23 Pamba v Toto Africans uwanja wa CCM Kirumba, Ndanda FC v Mshikamano Nagwanda Sijaona Mtara, huku Burkinafaso wakiwakaribisha Simba SC katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Januari 24, Young Africans watacheza dhidi ya Friends Rangers uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Njombe Mji v Tanzania Prisons uwanja wa Amani Makambako, mjini Shinyanga Stand United watachuana dhidi ya Mwadui FC.
Mechi zingine ni Kagera Sugar v Rhino Rangers, Panone v Madini, Mtibwa Sugar v Abajalo, Lipuli/Kurugenzi v JKT Ruvu, Ashanti United v Azam FC, Africa Sports v Coastal Union, Geita Gold v Mgambo Shooting, Singida United v Mvuvuma na Wenda v Mbeya City.
Timu 15 zilizofuzu hatua ya tatu kutoka raundi ya pili ni Ashanti United, Friends Rangers, Panone, Geita Gold, Pamba, Mvuvuma, Burkinafaso, Rhino Rangers, Madini FC, JKT Mlale, Mshikamano FC, Njombe Mji, Wenda FC, Singida United, Abajalo huku mchezo mmoja kati ya Lipuli dhidi ya Kurugenzi ukichezwa leo hii kusaka timu ya kufuzu raundi ya tatu.
Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) ataiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF CC) mwaka 2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni