.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 6 Januari 2016

WAZIRI MKUU ASEMA SERIKALI HAIJARIDHIA VIWANGO VIPYA VYA NAULI YA MABASI YAENDAYO KASI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haijaridhia viwango vipya vya nauli ya mabasi yaendayo kasi vilivyopendekezwa na waendeshaji wa huduma ya mabasi yaendayo kasi Dar es salaam (UDART).

Akizungumza leo na waandishi wa habari, mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku 3, Waziri Mkuu amesema Serikali haijaridhia viwango vipya vya nauli ya mabasi yaendayo kasi. Ambapo nauli ya kutoka Mbezi hadi Kimara shilingi 700, Mbezi hadi Kariakoo shilingi 1200, na nauli ya kutoka Mbezi hadi Mwenge shilingi 1400 na wanafunzi watatozwa nusu ya viwango hivyo vya nauli.

Waziri Mkuu amesema gharama hizi ni kubwa mno kwa wananchi na watumishi, mradi ulilenga kumrahisishia mtumishi wa Serikali anayeishi nje ya jiji, “Serikali iliwekeza katika mradi huu ili kusaidia watumishi na wananchi ambao hawana vipato vikubwa” alisema Waziri Mkuu.


Aidha, ameagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene na Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi, na Mawasiliano pamoja na wadau wakutane kupanga upya viwango hivyo na kama watashindwa basi Serikali itaendesha mradi huo.

Tarehe 25, Novemba 2015, Waziri Mkuu alimuagiza aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI na waendeshaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es salaam (UDART) kupitia misuada yote na kurekebisha miundombinu ili mradi huo wa mabasi uanze kufanya kazi ifikapo tarehe 10, Januari 2016, imebainika kwamba UDART hawakuandaa mpango wa biashara wala kuanisha gharama za uendeshaji.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMATANO, JANUARI 6, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni