.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 2 Februari 2016

UKULIMA BORA WA ZAO LA KARAFUU



Zanzibar ni maarufu kwa uzalishaji wa karafuu ulimwenguni kwa zaidi ya karne mbili zilizopita. Uzalishaji huo ulikuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia tani 35,000 mwaka 1830 na kumiliki soko la karafuu duniani kwa 90%.Iliongoza katika uzalishaji wa zao hilo kuanzia mwaka 1830 hadi 1940 kabla ya nafasi hiyo kuchukuliwa na Indonesia.
 

Tathmini iliyofanywa hivi karibuni ya Sensa ya miti (Woody Biomass Survey 2013) imeonesha kwamba Zanzibar kwa sasa ina idadi ya mikarafuu 4,131,783, ambapo Unguja pekee ipo jumla ya mikarafuu 277,196 na Pemba ipo mikarafuu 3,854,587.
 

Tathmini ya mwaka 1997 ilionesha idadi ya mikarafuu 790,400 kwa Unguja na mikarafuu 5,042,700 kwa Pemba (5,833,100). Hii inaonesha kupungua kwa idadi hiyo kwa asilimia 30 kwa idadi ya mikarafu ya Unguja na Pemba.
 

Pamoja na kuwa Karafuu ni Zao Kuu la Uchumi wa Zanzibar lakini hivi sasa ni nchi ya tatu duniani kwa usafirishaji wa karafuu, inatoa asilimia tano (5%) tu ya karafuu zinazozalishwa duniani.

Hali hiyo ilitokana na Sekta hiyo ya Karafuu kwa ujumla kukumbwa na changamoto nyingi kama vile ya kimasoko, uendeshaji na ukuaji wa sekta nzima. Serikali kwa kuzingatia umuhimu uliopo katika sekta hiyo, ilifanya tafiti mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto zilizopo.
 

Matokeo ya tafiti hizo zilipelekea kufanywa kwa mapitio ya Sheria zinazohusika na zao la karafuu. Matokea yake ni kupitishwa kwa sheria mpya ya ZSTC Namba 11 ya mwaka 2011, kupitishwa kwa Sheria Namba 2 ya Maendeleo ya Karafuu ya mwaka 2014 na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ikiwa ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuimairisha zao hilo.

Je kwa upande wa Wakulima wa zao hilo la karafuu wanatakiwa kufanya nini kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha zao hilo la uchumi wa Taifa na ustawi wa Wananchi?
 

Ili kuhamasisha Wakulima wanaimarisha zao hilo Shirika la ZSTC limeanzisha mashindano ya Wakulima na Wauzaji bora wa zao hilo ambapo kila Wilaya lazima apatikane Mkulima mmoja na Muuzaji mmoja bora ambapo huzawadiwa.
 

Je ni zipi Sifa za Mkulima Bora wa zao la Karafuu?.

Wataalamu wa Kilimo Bw. Badru Kombo Mwanvura kutoka Idara ya Misitu Unguja na Bw. Said Juma Ali Mkuu wa Idara ya Misitu Pemba wanatufahamisha mambo muhimu ambayo Mkulima anatakiwa ayazingatie katika kilimo cha zao la karafuu.
 

Ukubwa wa shamba

Inatarajiwa kuwa shamba kubwa linazalisha zaidi kuliko shamba dogo ingawa sio lazima iwe hivyo, inakisiwa kuwa shamba kubwa la karafuu ni kuanzia eka tatu (3) na kuendelea. Ukubwa wa shamba unatakiwa wende sambamba na wingi wa mikarafuu na uzalishaji wa karafuu kwa wingi.
 

Inatakiwa shamba liwe na mikarafuu angalau kwa asilimia themanini na tano (85%) kulingana na ukubwa wake.
 

Usafi wa shamba

Shamba la karafuu linatakiwa kuwa safi lote chini na lisiwe na pori linaloathiri mikarafuu wala lisizongwe na miti itambaayo. Vile vile liwe safi juu na wala lisiwe na miti itambaayo.
 

Pia shamba linatakiwa kusafishwa baada ya mavuno kwa kuondoa matawi yaliokatika na kuliweka katika mazingira mazuri kwa uzazi ujao.

Mkulima anatakiwa kupalilia baada ya kuchuma pamoja na kuhakikisha vitu vyote ambavyo si rafiki kwa mikarufuu vinaondoka ndani ya shamba. Kuliacha shamba katika hali ya uchafu kunaondoa ubora wa shamba.
 

Upandaji wa Mikarafuu Mipya

Katika uimarishaji wa zao la karafuu Mkulima anatakiwa awe na utaratibu mzuri wa kupanda mikarafuu kulingana na ukubwa na nafasi ya shamba lake. Inapendeza kuona shamba lina mikarafuu ya umri tofauti kama vile umri wa miaka mitatu (3), mine (4) na kuendelea.
 

Umbali wa mti na mti (“Spacing” metre) inatakiwa iwe mita 7 kwa 9 kwa mikarafuu ya kupandwa na metre 5 kwa mabotea. Unapopanda mikarafuu kwa kuipa nafasi, unatoa nafasi kwa mazao mengine kuweza kuoteshwa na kulipa ubora shamba. Hali hiyo pia hulipa shamba uweza wa kuwa na nafasi ya kupandwa mazao mengine ambayo husaidia katika kunawirisha na kustawisha mikarafuu.

Kuchanganya na Mazao Mengine

Mkulima wa zao la karafuu anashauriwa kupanda mazao ya muda mrefu na ya muda mfupi katika shamba lake la mikarafuu, kufanya hivyo kunasaidia kumpa hamu na muda Mkulima kulihudumia vyema shamba lake.
 

Inahofiwa kuwa shamba linapokuwa na mikarafuu mitupu huwa halipati uangalizi mzuri na Mkulima anaweza kulitelekeza shamba lake kwa sababu mikarafuu huanza kuazaa baada ya miaka mine (4) hadi mitano (5) na kwa msimu, hivyo Mkulima hukosa hamu na ari ya kulihudumia vyema shamba.
 

Mkulima anaweza kupanda mikarafuu na mazao mengine kama vile, mishokishoki, igililani, pilipilimanga, vanilla na migomba ndani ya shamba la mikarafuu ili kuisadia kivuli na kulipa uwezo wa kukua vizuri na kuongeza kipato zaidi.
 

Ubunifu wa Mkulima

Mkulima bora wa zao la karafuu anatakiwa kuwa mbunifu wa mbinu za kulitunza Shamba lake ingawa ni Wakulima wachache wenye kulifanyia kazi suala la ubunifu katika kilimo. Tafiti zinaonyesha kuwa Mkulima bora ni yule mwenye kubuni njia tafauti za kulifanya shamba lake liwe bora, Mfano kumwagilia maji na kuweka kivuli.
 

Kukabiliana na Maradhi

Mkulima anatakiwa awe na uwezo wa kukabiliana na maradhi ya mikarafuu kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo. Japokuwa tafiti zinaonesha ni mikarafuu michache inayopatwa na maradhi, lakini mabadiliko ya tabia nchi imekuwa ni changamto kubwa kwa ustawi wa mikarafuu. Wakati wa kiangazi ambapo huwa na jua kali na joto mikarafuu mingi hasa midogo hukauka.
 

Pia tatizo jengine ni mlangamia ambao hauna dawa zaidi ya Mkulima mwenyewe kuisafishia mikarafuu yake Ila Mkulima anashauriwa kuziona taasisi za kilimo au Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu pindi anapogundua matatizo katika mikarafuu yake ili waweze kufanya utafiti kugundua tatizo na kulitafutia dawa.
 

Ujenzi ndani ya Shamba.

Mkarafuu ni mti wenye maringo na nongwa sana hauhitaji usumbufu katika ukuaji wake. Unaweza kujenga kibanda au nyumba moja kwa ajili ya uangalizi wa shamba lakini si vyema kukata viwanja na kujenga nyumba za maakazi ya familia.
 

Kuwepo kwa maakazi ndani ya shamba la mikarafuu ni chanzo cha kufa na kudhoofika kwa mikarafuu kutokana na shughuli mabli mbali zinazofanywa na binadamu.
 

Umiliki wa shamba.

Shamba bora ni lile linalomilikiwa kihalali/kisheria na Mkulima, ni lazima liwe na hati ya utibitisho wa umiliki wake ili kuondoa migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza sana hasa baada ya kupanda kwa thamani ya zao la karafuu.
 

Umiliki wa shamba unaweza kuwa kwa kukodi, kuazimwa ama kupewa na serikali, kurithi na umiliki mwengine kwa njia za halali/kisheria, hivyo basi ili Mkulima wa zao la karafuu awe bora basi ni lazima shamba lake liwe na uthibitisho rasmi wa umiliki.

​​Makala hii inamazia kwa kutoa wito kwa Wakulima wa zao la karafuu kuendela kushirikiana na Serikali katika kuimarisha zao la karafuu ikiwa ni pamoja na kuuza karafuu zao katika Shirika la ZSTC ili kukuza uchumi wa Taifa ambao unategemea sana upatikanaji wa fedha za kigeni na kukuza ustawi wa Wananchi wote.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni