.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 3 Februari 2016

WANA CUF WAUNGA MKONO TAMKO LA BARAZA KUU LA UONGOZI LA CHAMA HICHO


                                                                                           Na: Hassan Hamad, OMKR

Wafuasi wa Chama Cha Wananchi CUF, wameunga mkono tamko lililotolewa na Baraza Kuu la Uongozi la Chama hicho la kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20/03/2016 Visiwani Zanzibar.

Wanachama hao kupitia viongozi wao wa Wilaya na Majimbo ya Unguja, wameunga mkono tamko hilo baada ya kupata maelezo ya kutosha kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia alikuwa mgombea Urais wa Zanzibar 2015, Maalim Seif Sharif Hamad, kwenye mkutano maalum kwa viongozi hao uliofanyika ukumbi wa Majid Kiembe Samaki Zanzibar.

Wamesema wameridhishwa na uamuzi wa Baraza Kuu, na kwamba hakuna sababu ya kushiriki uchaguzi huo ambao wamesema ni uchaguzi wa kulazimisha na hauwezi kuwa huru na wa haki.

Wameeleza kuwa uchaguzi halali, huru na wa haki ulishafanyika Oktoba 25, 2015 ambapo wananchi walio wengi walimchagua mgombea wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad lakini uchaguzi huo ulifutwa bila ya kuwepo sababu za msingi.

Mapema akizungumza na viongozi hao wa CUF ngazi ya Wilaya na Majimbo kwa upande wa Unguja, Maalim Seif amesema Chama hicho hakitorudi nyuma katika kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba 2015.

Amesema licha ya Chama hicho kutangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio, juhudi mbali mbali zinaendelea kufanywa kuhakikisha kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM kinaondoka madarakani.

Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar Maalim Seif amesema siasa za nguvu na kimabavu zinazoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi hazitoisaidia Zanzibar na badala yake zinaweza kuzidisha mgogoro uliopo.


Maalim Seif ameishutumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuingilia uchaguzi wa Zanzibar na kupelekea kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba.

Amesema saa chache kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo, kituo kikuu cha kutangazia matokeo kilichokuweko Hoteli ya Bwawani kilizingirwa na vikosi vya jeshi na polisi, na kukitaja kitendo hicho kuwa ni “Mapinduzi ya Kikatiba”.
 

“Aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu wakati ule alikuwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete, na ndiye aliyepeleka vikosi vile baada ya kuona Chama chake kimeelekea kushindwa kwa upande wa Zanzibar”, alisema Maalim Seif na kuongeza;
 

“Dkt. Shein wala Balozi Seif hawamiliki jeshi wala polisi, vile ni vikosi vya Dkt. Kikwete wakati ule na hawezi kukwepa lawama ya kuingilia uchaguzi wa Zanzibar”, alieleza.

Maalim Seif pia amewashutumu baadhi ya viongozi wakiwemo wa dini wanaojaribu kupotosha ukweli na kuunga mkono uamuzi batili wa kurejewa uchaguzi uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar. 

Akizungumzia kuhusu vikao vya kutafuta muafaka wa mkwamo wa kisiasa vilivyokuwa vikifanyika Ikulu ya Zanzibar, Maalim Seif amesema katika vikao hivyo walijadiliana na kukubaliana kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imepoteza sifa ya kusimamia uchaguzi, lakini ameshangazwa na kitendo cha Tume hiyo hiyo kutangaza uchaguzi wa marejeo, huku viongozi wa CCM walioshiriki mazungumzo hayo wakiunga mkono.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni