.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 12 Juni 2016

VIONGOZI WA MFUKO WA MAENDELEO YA PAMBA WAUMBULIWA

MKUU wa wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Ibrahimu Marwa amesema viongozi wa Mfuko wa Wakfu wa maendeleo ya zao la pamba uliwapelekea wakulima pembejeo feki na kuwasababishia hasara.

Amesema hatua hiyo inatokana wafanyabiashara na viongozi wa mfuko huo kuwa na maslahi binafsi katika zao la pamba hivyo kushindwa kuwasaidia wakulima ipasavyo.

Marwa aliyasema hayo jana (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga alipokuwa akisoma taarifa ya Mkoa huo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipowasili Mkoani hapo.

Alisema mara baada ya wakulima kupelekewa pembejeo hizo na kubaini kuwa na kasoro walizipeleka katika Kiituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukirigulu kilichoko mkoani Mwanza ambacho nacho kilithibitisha kuwepo kwa kasoro.

Kwa upande wake Waziri Mkuu amewataka Maofisa Kilimo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na kuwasaidia wakulima wa pamba ili waweze kupata tija.

Ametaka Maofisa Kilimo na viongozi wa maeneo yanayolima pamba kujipanga upya baada ya kumalizika kwa msimu wa mwaka kwa kuanza mikakati ya kufanya utafiti wa mbegu bora za pamba na kuziandaa za kutosheleza wakulima wote.

Alisema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na Maofisa Kilimo ambao wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa sababu mashamba ya wakulima yanashindwa kuendelea kwa kuwa hakuna mtu anayewafuatilia.

“Mwakani muanze kufanya utafiti kuanzia hatua za awali na kituo cha Ukirigulu kipewe kazi ya kusimamia zao hili na kiwe na shamba darasa kwa ajili ya kufundishia wakulima. Lengo ni kuhakikisha zao hili linakuwa na tija,” alisema.

Hata hivyo Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri za Wilaya zinazolima pamba zifanye utafiti ili kujua sababu zilizosababisha wakulima kupunguza ari ya kulima zao hilo.

Pia amewataka waachane na mfumo wa kilimo cha mkataba kwa sababu hauna tija kwa mkulima kwani hautengenezi ushindani na badala yake wajifunze mfumo unaotumika katika uuzaji wa zao la korosho.

(mwisho)

IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

JUMAPILI, JUNI 12, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni