.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 15 Januari 2017

BALOZI SEIF ASISITIZA KUWA MCHAKATO WA KUMPATA MGOMBEA URAIS KWA TIKETI YA CCM ULIOTUMIKA 2015 NDIO UTAKAOTUMIKA 2020

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akijumuika pamoja katika wimbo wa hamasa wa CCM ulioimbwa na Viongozi wa CCM Kata ya Mtoni Jimbo la Temeke na wale wa Kamati ya Ujirani Mwema ya Mkoa wa Magharibi Unguja wakati walipomtembelea Nyumbani Kwake Mtaa wa Kama.
Balozi Seif akizungumza na Viongozi hao katika kuwaasa kuwa na tahadhari ya kueleke njia salama ya kujiandaa katika harakati na maandalizi ya uchaguzi ndani ya Chama hicho.
Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mtoni Jimbo la Temeke Dar es salaam Bibi Khadija Said Mkwere akielezea mafanikio ya ziara yao wakati wa uwepo wao Visiwani Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujirani Mwema ya Mkoa wa Magharibi Unguja ambae pia ni Mjumbe wa NEC Nd. Keis Mashaka akitoa neno la shukrani katika Mkutano huo. Picha na – OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba wembe ule ule uliotumika katika mchakato wa kumpata Mgombea wa CCM katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Tanzania Mwaka 2015 ndio utakautumika katika kumpata Mgombea wa Chama hicho upande wa Zanzibar ifikapo uchaguzi wa mwaka 2020.

Alisema wembe huo ndio silaha pekee itayosaidia kusafisha virusi vitakavyojaribu kuibuka ndani ya chama hicho endapo yatatokea makundi yatayoashiria kutaka kukiyumbisha Chama hicho wakati utakapokaribia mchakato wa Uchaguzi huo.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo hapo Nyumbani kwake Kama wakati akizungumza na Viongozi wa CCM kata ya Mtoni Jimbo la Temeke Mjini Dar es salaam ambao wapo Zanzibar kwa mualiko wa wenyeji wao Kamati ya Ujirani Mwema ya Mkoa wa Magharibi Unguja kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za Maadhimisho ya kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema Chama cha Mapinduzi hakitawaonea haya wanachama wowote wenye sura mbili na itakapobidi italazimika chama hicho kusafisha taka taka hizo hasa katika kipindi hichi cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi ndani ya chama chenyewe.

Balozi Seif alisema inasikitisha kuona kwamba wapo Viongozi wa Chama hicho waliowahi kudiriki kununua kadi cha Chama na kuwapa baadhi ya Watu wengine wakiwemo wapinzani ili wawachague katika kura za maoni na hatimae wapinzani hao walitumia mwanya huo kuvuruga malengo na mikakati ya Chama cha Mapinduzi.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwakumbusha Viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi walazimike kufanya kazi ya ziada katika kuwabaini wanafiki hao wenye sura mbili wanazozitumia katika kutoa maamuzi yao wakati wa uchaguzi ndani ya Chama.

Akizungumzia Maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif alisisitiza kwamba masuala hayo yataendelea kuwa na umuhimu kwa Wazanzibari na Watanzania wote katika kujikumbusha mzizi wa fitina wa Kikolini uliokatwa na waasisi wa Mapinduzi hayo Mwaka 1964.

Balozi Seif alisema zaidi ya Miaka 200 iliyopita kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Wakwezi na Wakulima wa Visiwa vya Zanzibar walikuwa wakinyanyaswa kimaisha, madhila yaliyoamsha ari kwa Waasisi wa ASP kuandaa mipango ya kujikomboa kwa hali yoyote ile.

Aliwahakikishia Viongozi na wanacham hao wa CCM kwamba yale yote yaliyoasisiwa na Viongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kuhusiana na masuala ya Elimu, Afya na Eka Tatu Tatu walizopewa Wananchi bila ya malipo kuendesha maisha yao yataendelea kutekelezwa daima.

Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza Viongozi na Wananchama wa CCM Kata ya Mtoni Mjini Dar es salaam na wenyeji wao Kamati ya Ujirani mwema ya Mkoa wa Magharibi kwa uamuzi wao wa kuanzisha safari za ujirani Mwema unaowapa fursa za kutembeleana kila mwaka.

Alisema utaratibu waliouanzisha wa kutembeleana kwa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni vyemna wakaendelea kuudumisha kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Naye Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauti Kuu ya Taifa ya CCM Mama Asha Suleiman aliwaomba Viongozi na Wanachama wa CCM kuanza kufikiria suala la Uchaguzi wa Chama chao ambalo linastahiki kufanyiwa maandalizi ya mapema.

Mama Asha alisema ipo haja kwa Wana CCM kuwa makini katika kujiepusha mapema na migogoro iliyowahi kuleta sintafahamu wakati wa mchakato wa kumpata mpeperusha Bendera ya CCM katika maandalizi ya kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

Alisema tahadhari kubwa ni vyema ikachukuliwa katika kuyaondoa mapema magogo mabovu yaliyosababisha baadhi ya Viongozi na Wanachama wa CCM kujikwaa na kuleta usumbufu unaojenga mazingira mabaya ya ushindi mdogo wa Chama chao ambacho ndicho pekee chenye dhamira ya wazi ya kuyalinda Mapinduzi na kuduumisha Muungano uliopo.

Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania { UWT } Kata ya Mtoni Jimbo la Temeke ambae ndiye Kiongozi wa Msafara wa Viongozi hao kutoka Dar es salaam Bibi Khadija Said Mkwere alisema ziara ya ujumbe wake imetoa nafasi kubwa kujifunza mambo mbali ya Historia ya Zanzibar pamoja na ile ya Chama cha Mapinduzi.

Bibi Khadija Mkwere alisema ujo wao Visiwani Zanzibar mbali ya kuhudhuria Kilele cha Maadhimisho ya Sherehe ya kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia uliwapa fursa ya kushiriki katika kazi za Chama ikiwemo Mikutano sambamba na uzinduzi wa baadhi ya Maskani za CCM Visiwani Zanzibar.

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Wanawake Tanzania { UWT } Kata ya Mtoni Jimbo la Temeke koani Dar es salaam alielezea faraja yake katika kuona Heshima ya Tanzania inaendelea kukua kwa sababu ya uwepo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/1/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni