Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF), limetoa nafasi ya mwisho kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Jamhuri ya Congo (FECOFOOT) kumpeleka mchezaji Langa Lesse Bercy jijini Libreville, Gabon kwa ajili ya kipimo kipya cha MRI ili kutambua umri wake.
CAF limetaka FECOFOOT kumpeleka mchezaji huyo huko Libreville, Gabon ndani ya siku 10 zijazo kuanzia jana Januari 12, 2017.
CAF limepata kumwita mchezaji huyo mara mbili mwaka jana, na FECOFOOT imeshindwa kumpeleka kwa sababu mbalimbali wanazozijua FECOFOOT.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya kimataifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, vijana waliohitajika kucheza ni wale wenye umri wa chini ya miaka 17.
Langa Lesse Bercy, amelalamikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwamba amezidi umri hivyo kuhitajika kumpeleka kwani hakustahili kucheza hatua ya kufuzu kwa michuano hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.
Fainali za vijana zinatarajiwa kufanyika katika nchi nyingine itakayotangazwa hapo baadaye baada ya Madagascar kuondolewa kuandaa fainali hizo baada ya kubainika kutokamilisha baadhi ya taratibu.
Hii inatokana na ripoti ambayo CAF wameipata kutoka kwa wakaguzi wa maandalizi ya fainali hizo. CAF imefungua kandarasi ya kwa nchi wanachama wengine kuandaa fainali hizo. Mwisho wa kupokea maombi ni Januari 30, mwaka huu.
Kadhalika Kamati ya Utendaji ya CAF, imemteua Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Chilla Tenga kuwania nafasi ya uwakilishi katika Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Katika nafasi hiyo kutoka nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, Tenga atachuana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.
Wengine waliopitishwa kuwania nafasi ya uwakilishi katika Kamati ya Utendaji ya FIFA kutoka nchi za Afrika ni Tarek Bouchamaoui wa Tunisia ambaye anaingia kwenye kundi la nchi zinazozungumza lugha za Kiarabu, Kireno na Kihispaniola.
Kwa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa wamo Constant Omari Selemani wa DR Congo na Augustin Sidy Diallo wa Cote d’Ivoire wakati nafasi nyingine za wazi ihuhusisha mwanamke mmoja, wamo Almamy Kabele Camara (Guinea), Chabur Goc (South Sudan), Danny Jordaan (Afrika Kusini), Hani Abo Rida (Misri) na Lydia Nsekera (Burundi).
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni