Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma, 08 Feb 2017
Serikali imetolea ufafanuzi juu ya swala la michezo ya kubahatisha kuwa ni moja ya shughuli za kiuchumi, zinazoendeshwa kwa mujibu wa sheria kama shughuli zingine. Aidha michezo yote ya kubahatisha ikiwemo Kamari (slots machines) inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Michezo ya Kubahatiba Namba 4 ya mwaka 2003, Sura 41 pamoja na Kanuni zake.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Asha Abdullah Juma, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kudhibiti mchezo wa kamari ambao amesema huwakosesha amani wazazi na jamii nzima, kwa kuchangia uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya vijana inayopotea kwa kucheza kamari badala ya kushiriki katika uzalishaji.
Aidha, Dkt Kijaji, amesema kuwa kwa mujibu wa sheria, hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendelesha biashara ya Michezo ya Kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na vibali vingine vinavyotolewa na mamlaka zingine za biasahra. Vilevile , sheria inakataza watoto wenye umri chini wa miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.
“Mtu yeyote atakaye ruhusu mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la Mchezo wa Kubahatisha, anahesabika kafanya kosa na anastahili kulipia faini ya shilingi 500,000/- au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja” aliongeza Dkt. Kijaji
“endapo kosa hilo litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi ina mamlaka kisheria kumfutia leseni. Hivyo basi, wajibu wa Serikali ni kuzuia watoto na vijana walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha. Natoa rai kwa wazazi na walezi kuwazuia wao kucheza michezo hiyo” alisisitiza Dkt. Kijaji
Amewataka wote wanaoendesha michezo ya kubahatisha wazingatie sheria na kanuni zilizowekwa, huku akiwaangaliza wazazi na walezi na jamii kwa ujumla ihakikishe kuwa vijana wanazingatia mila na desturi zinazolinda maadili ya Kitanzania kwa kujishughulisha na shughuli halali za kiuchumi.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni