.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 27 Mei 2017

JUMIA TRAVEL YAZINDUA RIPOTI YA UTALII BARANI AFRIKA

KUZIDI kuongezeka kwa watumiaji wa intaneti barani Afrika na kufikia zaidi ya milioni 300 ambayo kiuwiano kwa ueneaji wake ni sawa na 27.7% ni ishara nzuri kwa uchocheaji wa ukuaji wa shughuli za utalii kwa njia ya mtandao.

Hayo yalibainishwa kupitia ‘Ripoti ya Utalii Afrika kwa mwaka 2017’ iliyowasilishwa na Jumia Travel inayojihusisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao, ambapo inaelezea kuwa teknolojia na huduma za simu zimeliingizia bara la Afrika mapato ya ndani kwa 6.7% kwa mwaka 2015 (ambazo ni sawa na dola za kimarekani bilioni 150 kwa thamani ya kiuchumi), na yanatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 210 (7.6% ya jumla ya pato la ndani la taifa) kufikia mwaka 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuiwasilisha ripoti hiyo, Meneja Mkaazi wa Jumia Travel nchini Tanzania, Bi. Fatema Dharsee amesisitiza kuwa takwimu hizo zinaifanya kampuni kuamini kuwa bara la Afrika lina fursa kubwa katika ukuaji wa sekta ya utalii kwa njia ya mtandao.

“Jumia Travel inaona kuwa ujio wa intaneti na kupokelewa vizuri na waafrika, ni ishara nzuri kwamba sekta ya utalii itakua ukizingatia ina mchango mkubwa kwenye kuchangia pato la taifa. 

Kwa mfano mpaka kufikia mwishoni wa mwaka 2015, 46% ya idadi ya waafrika (zaidi ya nusu bilioni ukilinganisha na idadi ya waafrika wanaofikia takribani bilioni 1.2) walijiunga na huduma za simu. Hii idadi ni ya kipekee kwani inatarajiwa kufikia milioni 725 mnamo mwaka 2020,” alisema Bi. Dharsee.

“Hayo yote kwa kiasi kikubwa yamechochewa na uapatikanaji wa mtandao wa intaneti wa 4G kwa zaidi ya nusu ya nchi za kiafrika, ambapo mpaka kufikia katikati ya mwaka 2016 takribani nchi 32 zilikuwa zimekwishaunganishwa na mitandao 72 ya LTE (Long-Term Evolution). 

Hata hivyo, bado tunajikongoja kwa namna tulivyopokea mabadiliko hayo ukilinganisha na sehemu zingine duniani ambapo ueneaji wake kwetu ni sawa na 20% ya idadi ya watu waliofikiwa na mtandao wa 4G,” aliongezea Menaja Mkaazi huyo wa Jumia Travel hapa Tanzania.

Aliendelea kwa kufafanua zaidi kuwa changamoto kubwa inayolikabili bara la Afrika kwa sasa hususani kusini mwa jangwa la Sahara ni ukosefu wa ujuzi kwenye masuala ya kigiditali. Hivyo basi wao wanaona kwamba kuunga mkono jitihada za utoaji elimu ya kidigitali kwa wadau wa utalii kuna umuhimu mkubwa katika kukuza sekta hiyo mtandaoni ndani ya bara la Afrika.

Mbali na uwasilishaji wa ripoti hiyo ya utalii barani Afrika pia kampuni hiyo imesema kuwa kwa sasa inaendesha kampeni inayolenga kuwakomboa waafrika kusafiri ndani na nje ya mipaka yao kwa gharama nafuu.

“Kampeni hii iliyopewa jina la ‘Democratize Travel’ dhumuni letu kubwa ni kuondoa mawazo yaliyojengeka miongoni mwetu haswa linapokuja suala la mchakato mzima kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hii inamaanisha kupunguza gharama hususani za malazi, upatikanaji wa taarifa pamoja na kutoa huduma bora kwa kila mtu. 

Pia kupitia kampeni hii tunataka kuwaonyesha wateja wetu uzuri uliofichika kuhusu bara la Afrika kwa kuwapatia suluhu ya mahitaji yao yote pindi wanapotaka kusafiri kama vile; hatua au mambo ya kuzingatia, malazi, chakula na shughuli za kufanya mahali waendapo,” alisema Bi. Dharsee.

“Hatutoishia hapo bali tunataka pia kuondoa mitazamo tofauti ya kwamba sehemu za kutembelea zilizopo nchi za Magharibi kama vile Ulaya na Marekani au Dubai ni bora zaidi ya Afrika. Mbali na kuwarahisishia waafrika kusafiri kwenye maeneo waliyopo lakini pia tunawawezesha kuvuka mipaka kwenda sehemu nyingine duniani. 

Hapa msafiri ataweza kulipia gharama za kusafiri, kwa mfano kwenda jijini London nchini Uingereza, kwa fedha ya nchi yake anayotokea. Hayo yote yanawezekana na yamerahishwa kwani kupitia mtandao wetu mteja ataweza kukatatiketi ya ndege na kufanya huduma ya malazi kwa sehemu anayokwenda kwa wakati mmoja,” alihitimisha Bi. Dharsee.

Kampuni hiyo imesema mbali na kuelekeza kampeni hiyo kwa wateja wake lakini pia itawashirikisha hoteli washirika katika kuhakikisha wanawafikia wateja na kukua kwa haraka zaidi. Hayo wanayahakikisha kupitia kuwatangaza mtandaoni ili kukuza muonekana na biashara zao, kuwapatia mifumo ya teknolojia inayoendana na soko la Afrika ili kuwarahishia uendeshaji wa biashara zao kama vile Extranet, SMS au barua pepe pamoja na kuchochea utoaji na uboreshaji wa huduma bora ili kuwavutia wateja wengi zaidi.

Akizungumzia namna Jumia Travel inavyorahisisha ufanyikaji wa shughuli za kila siku za hoteli, Kaimu Meneja Mkuu wa Hong Kong Hotel ya jijini Dar es Salaam, Bw. Mganja Suleiman amesema kuwa, “Kujiunga kufanya kazi na mtandao wa Jumia Travel kumetunufaisha kwa kiasi kikubwa sana ukilinganisha na hapo awali. 

Kwanza kabisa kujulikana na kutangazwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania hivyo kutuongezea soko, kama mjuavyo shughuli za matangazo na kutafuta masoko zinahitaji mfanyabiashara au kampuni iwe na fedha ya kutosha. 

Lakini kupitia mtandao huu wateja wanaweza kujua huduma tulizonazo bila ya hata kuwasiliana nasi moja kwa moja kwani kila kitu kipo mtandaoni na pia kuacha maoni yao pale wanapovutiwa na namna walivyohudumiwa au kitu gani cha kuboresha.”

“Kwa kiasi kikubwa mtandao huu umekuwa ni chachu kwa hoteli yetu kufanya vizuri na kuendelea kuboresha huduma zetu kwa ubunifu zaidi ili kuweza kumudu suhindani wa kwenye soko. 

Pia ningependa kutoa pongezi kwa kutuletea teknolojia mpya na za kisasa kabisa ambazo zinarahisisha kazi zetu. Kwa mfano mfumo wao wa Extranet ambao umelenga kuwarahisishia mameneja au wa hoteli au wapokeaji wa maombi ya huduma kutoka kwa wateja kwa njia ya mtandao popote walipo. 

Mfumo huu unapatikana kwenye kompyuta, tabiti na simu pia, hivyo kupunguza lile adha ya kumlazimu meneja kutoa huduma mpaka awe hotelini. Lakini pia mfumo huu unatupatia sisi fursa ya kujua aina, idadi na hadhi ya wateja wanaotumia huduma zetu hivyo kurahisisha kuwafikia na kuwapatia kile wanachokitaka,” alihitimisha Bw. Suleiman.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni