.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 27 Mei 2017

TIMU YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI YA SADC YAZINDULIWA LESOTHO

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), imesisitiza kuwa wapiga kura wa Lesotho wanatarajia kuwa Serikali itakayochaguliwa na wananchi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Wabunge wa mwaka 2017 itasimamia na kutekeleza mageuzi yanayohitajika nchini humo. 

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC, Kiongozi wa Timu hiyo Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema japo mazingira ya upigaji kura yameandaliwa na kukamilika, lakini huu ni uchaguzi wa tatu ndani ya miaka mitano na wapiga kura wamechoka. 

Ni matumaini ya SADC na ya wananchi wa Lesotho kuwa Serikali ijayo itajipanga vizuri na kusimamia kikamilifu mageuzi ya kikatiba na kimfumo ambayo yataleta uimara wa kisiasa na unaotabirika nchini humo.

"Jumuiya yetu imejiwekea misingi imara ya kidemokrasia ambayo ikijumuishwa na ile ya nchi, na kimataifa kama Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa tunapata vigezo tisa ambavyo timu yetu itaviangalia wakati huu wa uchaguzi" alisema Balozi Mahiga.

Baadhi ya vigezo vitakavyoangaliwa kwenye uchaguzi huo ni ushiriki wa wananchi kwenye michakato ya siasa, fursa sawa kwa vyama vyote vya siasa, uhuru wa taasisi zinazosimamia uchaguzi, elimu ya mpiga kura na wajibu wa wagombea na vyama vya siasa kukubaliana na matokeo kama yatakavyotangazwa na tume huru ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi husika.

Wadau mbali mbali waliohudhuria hafla hiyo wakiwemo Viongozi wa vyama vya Siasa na Jumuiya ya Diplomasia nchini Lesotho, walielezwa kuwa SADC imepongeza hatua ya vyama vya siasa kuweka makubaliano yaliyosainiwa na Viongozi wa vyama kukubali matokeo ya uchuguzi iliyoratibiwa na Umoja wa Makanisa Lesotho.

Uchaguzi Mkuu wa Wabunge nchini Lesotho unatarajiwa kufanyika tarehe 3 Juni 2017 ambapo Chama au Muungano wa Vyama vyenye ushindi mkubwa wa viti vya ubunge, wataunda Serikali ambayo itaingozwa na Waziri Mkuu.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Maseru, Lesotho 26 Mei, 2017

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni