.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 14 Juni 2017

WANAFAMILIA WAALIKWA KUCHUKUA FOMU TFF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linawaalika wanafamilia wote wenye nia ya kuwania uongozi katika shirikisho kujitokeza kuchukua fomu kuanzia Juni 16, mwaka huu.
 

Tarehe hiyo ni ileile iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Revocatus Kuuli alipozungumza na wanahabari Jumatatu wiki alipotangaza ratiba nzima ya Uchaguzi Mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
 

Kwa kuwa tovuti ya TFF: www.tff.or.tz kwa sasa ipo kwenye marekebisho, zoezi la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi TFF zitatolewa kwenye ofisi za TFF zilizopo Ilala, Dar es Salaam kuanzia asubuhi ya Juni 16, 2017 hadi saa 10 jioni siku ya Juni 20, mwaka huu.
 

Fedha za kulipia fomu hizo zitalipiwa Benki ya CRDB kupitia namba ya akaunti 01J1019956700 ambako mgombea atawajibika kuwasilisha stakabadhi ya malipo kutoka benki na kupewa fomu ya nafasi husika.
 

Gharama za kuchukulia fomu ni.

1. Rais TSHS 500,000/=

2. Makamu wa Rais TSHS 300,000/=

3. Wajumbe wa kamaki ya utendaji TSHS 200,000/=
 

MAYANGA ATANGAZA TAIFA STARS YA COSAFA
 

Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Shabani Mayanga, leo Jumatano Juni 14, 2017 ametangaza majina ya wachezaji 22 watakaounda kikosi kinachokwenda kushindana kuwania Kombe la Castle Cosafa nchini Afrika Kusini.
 

Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, inatarajiwa kuanza kambi rasmi kesho Jumapili Juni 18, mwaka huu. Kambi hiyo itakuwa kwenye Hoteli ya Urban Rose, iliyoko Mtaa wa Jamhuri katikati ya jiji la Dar es Salaam.
 

Taifa Stars inajiandaa na michuano ya Cosafa inayotarajiwa kuanza Juni 25, mwaka huu. Michuano hiyo, inaandaliwa na Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika ambako Tanzania - mwanachama wa Cecafa, imepata mwaliko kushiriki.
 

Tanzania imepangwa kundi A ambako wapinzani wake ni Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland zitakuwa na mechi maalumu (play off) ili kuingia robo fainali.
 

Kwa mujibu wa Mayanga, kikosi hicho kinaundwa na makipa Aishi Salum Manula (Azam FC), Benno David Kakolanya (Young Africans SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC). 

Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Salum Kapombe (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Young Africans SC) wakati upande wa kushoto wapo Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto Africans FC).
 

Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.
 

Kadhalika wako viungo wa kushambulia ambao ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba SC).
 

Katika safu ya ushambuliaji wamo Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).
 

UTARATIBU MPYA WA USAJILI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI WAJA
 

Baada ya kufutwa utaratibu wa mawakala ‘agents’ wa wachezaji wa kulipwa, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), lilitangaza utaratibu mpya wa kukasimu majukumu hayo kwenye ngazi ya mashirikisho kwa kila taifa.

Hivyo kwa mwaka 2016/2017, hakuna usajili wala uhamisho uliofanywa na watu wa kati yaani intermediaries wanaotambulika na TFF.

TFF - Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, linakwenda sambamba na utaratibu huo wa mabadiliko na kwa sasa linakamilisha mipango ya kusajili watu wa kati wa usajili watakaofahamika kama intermediaries.

Usahili wa kati utatangazwa baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kitakachojadili kanuni za watu wa kati hapo baadaye.
 

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni