Daktari Mkuu wa
Hospitali ya Abdullah Mzee Dr. Haji Mwita Haji Kulia akimtembeza
sehemu mbali mbali za Hospitali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kukagua huduma za afya
wanazopatiwa Wananchi mbali mbali Hospitalini hapo.
Mkuu wa Kitengo
cha X Ray katika Hospitali ya Rufaa ya Abdullah Mzee iliyopo Mkoani
Pemba Dr. Muhsin Aley Ali Kulia Kimpatia maelezo Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kukagua huduma za
uchunguzi wa Afya Hospitalini hapo, wa kwanza kutoka Kushoto ni
Daktari Mkuu wa Hospitali ya Abdullah Mzee Dr. Haji Mwita Haji.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishiriki shughuli za
uhamasishaji wa uchumaji wa Zao la Karafuu katika Mbiji Changaweni
Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Mhandisi
Muelekezi wa Kampuni inayosimamia ujenzi wa Ofisi Tatu za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar Mtaa wa Gombani Chake chake Pemba Bwana
Mbarouk Juma Mbarouk akimpatia maelezo Balozi Seif aliyefika kukagua
maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Ofisi hiyo.
Mhandisi Mbarouk
akimkaguza Balozi Seif katika maendo mbali mbali ya ndani ya majengo
yanayoendelea kujengwa hapo Gombani yatakayozijumuisha Wizara Tatu za
Fedha, Katiba na inayosimamia Wanawake na Watoto. Picha na OMPR-
ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kuchukuwa hatua za kisheria kwa kutaifisha Karafuu
zinazotoroshwa Nchini sambamba na kukichoma moto mara moja chombo
kitakachohusika kutaka kusafirisha zao hilo.
Alisema hatua hiyo ya awali ambayo
ni miongoni mwa Mikakati ya Serikali ya kukabiliana na magendo ya
Karafuu itafuatiwa na wahusika wa utoroshaji wa zao hilo kushikisha
katika vyombo vya sheria kwa kuhusika na uhujumu wa Uchumi wa Taifa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo
hilo wakati wa shughuli za uhamasishaji wa uchumaji wa zao la karafuu
karafuu hapo katika Kijiji cha Mbiji Changaweni Wilaya ya Mkoani
akimalizia ziara yake ya siku mbili Kisiwani Pemba kukagua shughuli
za Maendeleo.
Alisema kwa vile Karafuu bado
zinaendelea kuwa ndio mtaji Mkuu wa mapato ya Taifa Serikali kamwe
haitovumilia wala kukubali kuona vitendo vya magendo ya Karafuu
kutoroshwa nje ya Nchi vinaendelea kwa tamaa za Watu wachache.
Balozi Seif alisema tabia hiyo mbovu
ya kutorosha mali ya Taifa haimsaidii mtu bali ni kuikosesha Serikali
Mapato jambo ambalo athari yake huonekana pale baadhi ya huduma
zinapokosekana kutokana na uhaba wa Mtaji wa Serikali unaotokana na
chanzo hicho cha Magendo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alisisitiza Wananchi hasa Wakulima wajitahidi kuzichuma Karafuu zote
zilizozaa katika Msimu wa Mwaka huu na baadae kuziuza katika vituo
cha Shirika la Taifa la Biashara { ZSTC
Akitoa Taarifa za maandalizi ya
Uchumaji wa zao la Karafuu kwa Msimu wa Mwaka huu wa 2017/2018 kwa
niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar,
Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Kisiwani Pemba Nd. Abdullah Juma Khamis
msimu wa uchumuaji waq zao hilo bado haujachanganya vyema.
Nd. Abdulla alisema uvunaji halisi
wa zao hilo uliozinduliwa mnamo Tarehe 24 Julai 2017 unatarajiwa
kuchanga vizuri baada ya kukamilika kwa Mwezi Mmoja ujao.
Alisema Shirika la Taifa la Biashara
Zanzibarv {ZSTC}limeshajiandaa
kwa mtaji pamoja na vifaa ili
Karafuu zote zitakazochumwa ziuzwe
kwenye Shirika hilo kwa mujibu wa
Sheria na Taratibu za Nchi.
Afisa Mdhamini huyo Wizaraya
Baioshara, Viwanda na Masoko alifahamisha
kwamba ununuzi wa zao la Karafuu
umeshaanza tokea Tarehe 17 Julai 2017
na tayari Tani zipatazo 97.3
zimeshanunuliwa zikiwa na thamani ya
Shilingi za Kitanzania Bilioni 1.4.
Nd. Abdullah kupitia shughuli hiyo
ya uhamasishaji wa uchumaji wa zao
la Karafuu amewakumbusha na kutoa
wito kwa Wakulima wazingatie
uchumaji, uchambuaji pamoja na
uanikaji mzuri unaozingatia na kukidhi
viwango vya soko la Kimataifa.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Nd.
Hemed Suleiman Abdullah alisema
Mashamba ya Serikali yapatayo 366
yameshakodishwa kwa Wafanyabiashara
mbali mbali na kuiingizia Mapato
Serikali Kuu zaidi ya Shilingi
Milioni 66,000,000/-.
Alisema ukodishwaji huo umezingatia
zaidi kivuja jasho cha Wakulima
waliojitolea kuyatunza Mashamba ya
Serikali kwa kupewa upendeleo wa
ukodishwaji wa Mashamba ya Karafuu
kwa kupunguziwa asilimia ya Fedha
wanazokodishwa.
Nd. Hemed alisema changamoto liliopo
hivi sasa kwa baadhi ya Mashamba
ya Serikali ambayo yalikuwa
yakihodhiwa na baadhi ya Watu kwa muda
mrefu ni kuendelea kutumiwa kwa
Nyaraka zilizofuta mara baada ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya ya
Mkoani alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kwamba Kamati
iliyoundwa na Serikali kuyagundua na
baadaye kuyahakiki Mashamba yote ya
Serikali imebaini baadhi ya
mashamba hayo yameshauzwa kienyeji
bila ya kufuatwa kwa taratibu.
Alisema Kamati hiyo tayari
imeshachukuwa hatua za kuwanyang’anya
Mashamba baadhi ya Watu waliokuwa
wamejimilikishwa kinyume na taratibu
hizo na kuyarejesha Serikalini na
kuwataka Watu waliouziwa kudai fedha
zao kwa waliowauzia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif katika ziara yake pia
alikagua maendeleo ya ujenzi wa
Majengo ya Wizara Tatu za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar unaoendelea
katika Mtaa wa Gombani Chake Chake
Pemba.
Mhandisi Muelekezi wa Mradi wa
Ujenzi wa Majengo hayo kutoka Kampuni
ya Quality Building Contructor Bwana
Mbarouk Juma Mbarouk alimueleza
Balozi Seif kwamba ujenzi huo
unazingatia umakini mkubwa ili kuepuka
kasoro ndogo ndogo zinazoweza
kujitokeza kutokana na mazingira halizi
ya ardhi ya sehemu hiyo.
Bwana Mbarouk alisema Majengo hayo
ya ghorofa Tatu Tatu yanazijumuisha
kwa pamoja Wizara ya Ajira,
Uwezeshaji Wananchi, Wazee, Vijana
Wanawake na Watoto, Wizara ya Fedha
na Mipango pamoja na Wizara ya
Nchi Ofisi ya Rais, Sheria Katiba,
Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Alisema Afisi hizo ambazo kila
Wizara itakuwa na Ngazi yake
inatarajiwa kuwa na Ofisi 150, kumbi
Tatu za Mikutano kwa kila Wizara
pamoja na ule Mkubwa utakaokuwa na
uwezo wa kuhudumia Watu 400 kwa
wakati mmoja.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar aliridhika na
hatua ya ujenzi wa majengo hayo
yanayoonyesha kiwango kinachokubalika
hasa kutokana na Maamuzi ya Kampuni
ya ujenzi huo kuamua kufyatua
matofali yake wenyewe ili kuepuka
udanganyifu unaoweza kuharibu sifa
ya Kampuni hiyo.
Mapema asubuhi Balozi Seif alikagua
Huduma za Afya zinazotolewa
katika Hospitali ya Rufaa ya
Abdullah Mzee iliyopo Mkoani na kuridhika
na juhudi kubwa inayochukuliwa na
Madaktari na wafanyakazi wa
Hospitali hiyo.
Hata hivyo balozi Seif aliutaka
Uongozi wa Wizara ya Afya kuhakikisha
kwamba unazifanyia kazi baadhi ya
changamoto zinazoikabili Hospitali
hasa upungufu wa Madaktari Bingwa wa
maradhi mbali mbali, ukamilishaji
wa baadhi ya Vifaa pamoja na Haki za
Wafanyakazi wake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni