Usajili wa timu za Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili
kwa msimu wa 2017/18, umekamilika kwa timu 62 tu na timu mbili
zimeshindwa kufanya usajili.
Tayari toleo la awali (First Draft)
la majina ya timu zote na namna zilivyosajili, tumebandika katika
mbao za matangazo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Karume Dar es Salaam tangu jana na kusamazwa kwa vyombo vya habari.
Kubandikwa huko na kusambaza kwenye
vyombo vya habari kunalenga kuwapa fursa timu zote kukagua majina ya
wachezaji wa kila timu ili kuona kama kuna klabu au mchezaji amefanya
udanganyifu wa kusajili wa timu zaidi ya moja, ziweze kuona.
Kama kuna dosari hiyo, TFF imefungua
milango ya kupokea pingamizi la usajili wa wachezaji hao kuanzia leo
Agosti 8, 2017 hadi Jumatatu Agosti 14, mwaka huu saa 10.00 jioni
(16h00).
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za
Wachezaji inatarajiwa kuwa na kikao ama Agosti 16 au 17, mwaka huu
kupitia mapingamizi hayo pamoja na usajili wa timu za Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara. Usajili wa timu za Daraja la Kwanza na Pili,
utapitiwa baadaye mwezi huu.
Timu hizo 62 kati ya 64 zimefanya
usajili na kuingiza majina ya wachezaji, viongozi wa benchi la ufundi
kwenye mfumo wa mtandao wa TMS - Transfer Matching System.
Timu ambazo zimeshindwa kufanya
hivyo yaani usajili kwa mfumo wa TMS ni za Ligi Daraja la Pili (SDL)
ambazo ni Pepsi ya Arusha na Bulyanhulu ya Shinyanga.
Na kwa msingi huo, timu hizo za
Pepsi na Bulyanhulu zimejitoa kushiriki ligi kwa msimu wa 2017/18 na
zinashushwa daraja hadi ligi ya wilaya kuanza upya kutafuta nafasi za
juu kupanda daraja.
……………………………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA
MIGUU TANZANIA
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni