
Mkuu wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu amewataka wananchi na watendaji wa serikali, kuhakikisha wanashiriki na kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maji ili kutatua kero ya maji wilayani humo.
Babu ametoa kauli hiyo hii leo wakati akizungumza kwenye hafla ya kusaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa kutatua kero ya maji wilayani Serengeti, baina ya shirika la Amref Tanzania na halmashauri ya wilaya hiyo.
Mradi huo ujulikanao kama “Rain Tanzania” unatekelezwa wilayani humo kwa kipindi cha miaka miwili kupitia ufadhiri wa taasisi ya Cocacola Afrika katika Kata za Mosongo, Kenyamonta, Busawe pamoja na Nyansurura, ukilenga kusaidia upatikanaji wa majisafi na salama karibu na makazi ya wananchi ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu dolla za Marekani sita.
Meneja wa mradi huo, Mhandisi Japhet Temu amesema pia utasaidia kuhamasisha usafi wa mazingira, ujengaji na utumiaji wa vyoo bora pamoja na kuwawezesha kiuchumi vijana na akina mama ambapo vikundi 50 vya vijana na 20 vya akina mama vitawezeshwa mafunzo na mitaji ya ujasiriamali.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Mkazi wa Amref Tanzania, Mturi James amewahimiza wananchi kushiriki vyema kwenye utekelezaji na utunzaji wa miundombinu ya mradi huo ili kuhakikisha unakuwa endelevu.
“Ndoa nyingi zinapata shida pale ambapo wanawake wanakwenda kuchota maji umbali mrefu na kuchelewa kurudi nyumbani”. Anasema Bi.Bwiru Elisha, mkazi wa Kijiji cha Gantamome wilayani Serengeti.
Wilaya ya Serengeti inakabiliwa na kero ya upatikanaji wa maji ambapo Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mhandisi Juma Hamis anasema kati ya miradi 10 ya maji katika halmashauri hiyo, ni miradi miwili pekee imekamilika na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Mhandisi wa maji katika halmashauri ya wilaya ya Serengeti, Dickson Protas anasema wastani wa matumizi ya maji kwa kila mwananchi ni lita tano kwa siku ingawa uhitaji ni wastani wa lita 30 katika maeneo ya vijijini na lita 65 hadi 70 katika maeneo mjini.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni