WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaomba Watanzania waendelee kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwl.
Julius Nyerere kwa kuiga maisha yake na utendaji wake.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Oktoba
14, 2017) aliposhiriki ibada maalumu ya kumuombea Mwl. Nyerere
iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Minara Miwili Zanzibar.
Ibada hiyo ya kumbukumbu ya miaka 18
ya kifo cha Mwl. Nyerere ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Mbio
za Mwenge wa Uhuru uliozimwa leo katika mkoa wa Mjini Magharibi
visiwani Zanzibar.
Katika Idaba hiyo Waziri Mkuu
amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanamuenzi Mwl. Nyerere kwa
kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.
Awali, Katibu wa Jimbo Katoliki
Zanzibar Padri Cosmas Shayo ambaye aliongoza ibada hiyo aliwaomba
waamini wamuenzi Mwl. Nyerere kwa kudumisha umoja na mshikamano wa
Taifa.
“Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere
aliwapenda watu wote bila kujali Imani zao wala itikadi zao. Alikuwa
mzalendo na alitaka Watanzania waishi maisha bora.”
Padri Shayo aliongeza kuwa tunu za
amani na umoja zilikuwa miongoni mwa falsafa kuu ya Mwl. Nyerere,
ambapo matokeo yake ni umoja na mshikamano wa Taifa uliopo.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na Makamu wa
Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Seif Ally Idd, Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu, Bi Jenista Mhagama, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa.
Wengine ni Waziri wa Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Bi. Mauldine Castico,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako,
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira Bw. Anthony
Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Walemavu Bi. Stella Alex
Ikupa na mwakilishi wa familia ya Mwl. Bw. Makongoro Nyerere.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, OKTOBA 14, 2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni