.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 15 Novemba 2017

MAAFISA AAKIA WAFURAHISHWA NA ULINZI JNIA

Na Mwandishi Wetu

MAAFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.

Maafisa hao kutoka Idara mbalimbali walitoa kauli hiyo leo katika ziara ya siku moja ya mafunzo JNIA, ambapo walitembelea maeneo mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa husika.

Mkuu wa msafara wa maafisa hao, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Bw. Shaaban Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya msingi ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, pia wamejifunza namna abiria na mizigo anavyokaguliwa kwa kutumia mitambo ya kisasa kabla ya kupanda ndege.

Bw. Kombo alisema JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo pia katika upande wa utoaji wa vitambulisho wamejifunza namna utoaji wa vitambulisho unavyofanyika, ambapo AAKIA hutoa vitambulisho vya kudumu mara utaratibu wa muombaji utakapokamilika, tofauti na JNIA muombaji anaweza kupewa kitambulisho cha muda na kuendelea kufanyakazi huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo.

“Tumefaidika na mambo mengi ukiangalia sisi kwetu hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila kwetu kwa kipindi chote mteja anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea na kazi zake eneo la kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa na cha muda kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo,” alisema Bw. Kombo.

Naye Mkuu wa kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha JNIA, Bw. Lugano Mwansasu alisema ziara ya maafisa wa AAKIA imewafariji na kuanza ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano, ambapo nao wamejifunza kulingana na maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.

Bw. Lugano alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuiga mfano huu wa kupeleka maafisa wake kwenye viwanja mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza utendaji kwa lengo la kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.

“Kila siku mambo ya uendeshaji yanabadilika, basi tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu tujifunze huko, zipo changamoto labda sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu kutoka kwa wenzetu,” alisema Bw. Lugano.

Katika hatua nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA, Bw. Vedastus Fabian alisema faida ya ziara ya mafunzo ni kujijengea uwezo na mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na kingine.

Bw.Fabian alisema ziara hizo zinasaidia katika kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege, ambapo kwa sasa kumekuwa na masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na nyara za serikali.
 Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia), akitoa maelezo kwa Maafisa wa Idara mbalimbali kutoka kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA) waliofanya ziara ya mafunzo. Kushoto ni Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama JNIA, Bw. Hamis Mashaka.
 Maafisa wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), Bw. Shaaban Kombo (kuanzia wa pili kulia), Bi. Zakhia Mohamed, Bw. Salehe Said na Bi. Fatma Yussuf wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia) akiwaelekeza jambo wakati wa ziara yao ya mafunzo iliyofanyika leo.

 Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Hamis Mashaka (kushoto), akitoa maelezo mbalimbali yanayohusiana na ulinzi na usalama kwa maafisa kutoka idara mbalimbali za Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) cha Zanzibar walipofanya ziara ya mafunzo leo.
 Meneja Uendeshaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Vedastus Fabian (kulia) akiwapa maelezo mbalimbali Maafisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) walipofanya ziara ya mafunzo leo.
Afisa Habari katika jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (VIP-JNIA), Bw. Kenny Kwenga (kushoto) akitoa maelezo ya namna watu mashuhuri wanavyohudumiwa kwa maafisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA), walipofanya ziara leo. Kulia ni Msimamizi wa VIP, Bi. Josephine Mwaisukule.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni