.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 8 Desemba 2017

BALOZI SEIF AZINDUA MASHINDANO YA TAIFA YA MICHEZO YA WATU WENYE ULEMAVU WA AKILI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Wazazi wenye Watoto walemavu ambao huwashirikisha Watoto wao kwenye Michezo tofauti kuchukuwa jitihada za makusudi za kuwaelimisha Wazazi wenzao wenye Watoto kama hao kuwajumuisha katika michezo na shughuli mbali mbali zinazowahusu.

Alisema michezo mbali mbali wanaoshirikishwa Watoto hao wenye mahitaji maalum mara nyingi husaidia kuleta marekebisho endelevu ya tabia na mienendo ya Watu wenye ulemavu wa akili kutokana na kuwa michezo ni tiba.

Akizindua rasmi mashindano ya Taifa ya Michezo ya Watu wenye Ulemavu wa Akili { Special Olympics } huko Uwanja wa Aman Mjini Zanzibar Balozi Seif alisema Wananchi lazima wabadili misimamo na mitazamo yao jinsi wanavyowaona na kuwachukulia watu wenye ulemavu wa akili.

Balozi Seif alisema walemavu ni Binaadamu kama walivyo wengine ambao wana uwezo na hata vipaji vya kufanya mambo mengi makubwa na ya ajabu endapo watapatiwa fursa za kutumia vipaji na ujuzi waliobarikiwa.

Alisema Watu wenye ulemavu hasa wa akili kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa haki zao za msingi kutokana na mitazamo hasi iliyomo katika Jamii juu ya mazingira yao.

Alieleza kwamba Serikali zote mbili Tanzania zitaendelea kupambana na mitazamo hiyo hasi kwa kuendelea kuwaelimisha Wananchi pamoja na kujenga mazingira mazuri zaidi kupitia sheria, sera na mikakati kwa Watu wenye Ulemavu wa akili ili kupata haki zao za msingi kama Watu wengine.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kupitia mashindao ya Michezo mbali mbali ya Kimataifa ya Watu wenye ulemavu Vijana wa Tanzania wamekuwa wakililetea sifa Taifa kutokana na ushiriki wao uliowawezesha kuibuka na Medali mbali mbali kwenye mashindano hayo.

Balozi Seif alisema mafanikio hayo yanamaanisha kwa wasimamizi wa michezo husika hawana budi kuandaa mashindano ya Kitaifa kwa kuzingatia vigezo vilivyopo Kimataifa ili Timu ya Taifa ya Tanzania iendelee kushinda tuzo mbali mbali.

Alifahamisha kwamba Serikali kwa upande wake itakuwa tayari kuhakikisha Vijana wanaochaguliwa kuiwakilisha Nchi katika mashindano ya Dunia wanaandaliwa vizuri ili wazidi kuliletea sifa Taifa kupitia Michezo hiyo.

Balozi Seif aliwakumbusha Wanamichezo Nchini faida zinazopatikana ndani ya Jamii kutokana na uwepo wa mashindano mbali mbali ikiwemo michezo ya Watu wenye ulemavu wa akili.

Alizitaja baadhi ya faida hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa mtazamo zaidi wa Jamii juu ya uwezo walionao watu wenye ulemavu wa akili na kuongeza upatikanaji wa haki ya ushirikishwaji katika shughuli za Maendeleo sambamba na kudumisha Muungano kwa kuzingatia wanamichezo wanaoshiriki wanatoka Mikoa zaidi ya 30 Tanzania.

Alisema Sekta ya Utalii ambayo ndio tegemeo kubwa kwa Uchumi wa Taifa pia inajikuta ikitangazwa kupitia mashindano hayo ambapo kipato cha Taifa na hata watu wa kawaida huongezeka na kusaidia azma ya Serikali ya kupunguza umaskini kwa Wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza waandaaji wa mashindano ya michezo ya Watu wenye ulemavu wa akili kwa jitihada walizochukuwa za kuwashindanisha wanamichezo hao licha ya changamoto nyingi walizopambana nazo ikiwemo ukosefu wa wadhamini na wafadhili wa kutosha.

“ Kwa kweli michezo hii { Special Olympics } ndio kwa kiasi kikubwa inayotupatia sifa kubwa Duniani”. Alisema Balozi Seif.

Alisema wadhamini wengi wanaona kuwa michezo ya watu wenye ulemavu haiwezi kuwatangaza, jambo ambalo sio sahihi, Special Olympics inaweza kuwatangaza kama ilivyo michezo mengine Nchini.

Akitoa Taarifa ya Mashindano hayoMkurugenzi wa Special Olympics Tanzania Chales Rais alisema michezo hiyo imeanzishwa katika misingi ya kuwaandaa watu wenye ulemavu hasa Watoto kushiriki katika matukio na shughuli za amali kama watu wengine.

Hata hivyo Charles alieleza kwamba bado ipo changamoto kubwa inayowakabili Watu wenye ulemavu wa akili ya unyanyapaliwa kutoka kwa baadhi ya watu na hatimae unapelekea kukoseshwa haki zao za kupata Elimu, ushiriki wa michezo sambamba na mchanganyiko ndani ya Jamii katika mazingira ya kutafuta maisha.

Charles alisema mashindano ya mwaka huu ya Special Olympics ambayo yameshiriksha wanamichezo 650, Makocha 100 na Valantia 50 kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki katika mashindano ya michezo ya Soka, Riadha na Mpira wa Wavu.

Mkurugenzi huyo wa Special Olympics Tanzania kupitia Kamati na uongozi wa Mashindano hayo wameishukuru Kampuni ya Kizalendo ya Azam kwa kudhamini mashindano hayo ikiwemo Tiketi za Usafiri wa Boti pamoja na uchapishaji wa T. Shirts za mashindano hayo.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuyazindua mashindano hayo ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Mwenyekiti wa Special Olympics Tanzania Dr. Mwanandi Swed aliziomba Serikali zote mbili Nchini Tanzania kuandaa Bajeti maalum kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu wa Akili ili zisaidie harakati zao za kila siku ikiwemo shughuli za Michezo.

Dr. Mwanandi alisema hicho ni kilio cha muda mrefu kinacholiliwa na kundi la Watu wenye mahitaji Maalum hasa lile ya Michezo ya Olympics ambapo halijawa kupatiwa fungu ndani ya Bajeti za Taasisi za Umma tokea kuasisiwa kwa Michezo hiyo Mnamo Mwaka 1988.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akipokewa na Viongozi wa Special Olympics alipofika uwanja wa Aman Mjini Zanzibar kuyazindua Mashindano ya Taifa ya Michezo ya Watu wenye Ulemavu Tanzania.
Balozi Seif akipewa zawadi Maalum ya Vijana washiriki wa Special Olympics wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mashindano ya Taifa ya Michezo ya Watu wenye Ulemavu Tanzania yanayofanyika katika Uwanja wa Amani.
Baadhi ya Washiriki wa Special Olympics Tanzania wanaowakilisha Mikoa yao kwenye mashindano ya Michezo ya Watu wenye Ulemavu inayofanyika katika Uwanja wa Aaman kwa muda wa siku Tatu.
Vijana Wenye ulemavu kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar wanaoshiriki mashindano ya Special Olympics wakifuatilia uzinduzi wa mashindano hayo ambapo Mgenio Rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Picha na – OMPR – ZNZ.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni