Prof. Mbarawa alisema leo wakati alipoongea na wadau hao kwenye ukumbi wa watu Mashuhuri wa JNIA-TBII, wakati walipozungumza nao kujadili masuala mbalimbali.
Alisema baadhi ya wadau wameshalipa madeni yao kati ya bil 10 zilizokuwa zinadaiwa na sasa zimesalia bil. 3.7 ambapo amewataka baada ya kumalizika kwa sherehe za Krismas na Mwaka Mpya wahakikishe wanakamilisja madeni yao.
“Hatutasita kumuondoa mtu yeyote atakayekuwa akiendelea kudaiwa kwani atakuwa hana sifa za kupangisha katika majengo haya ya viwanja vya ndege kwa kuanzia TBI na hapa TBII,” alisema Prof. Mbarawa.
Hatahivyo, aliyapongeza mashirika na ofisi ambazo zimekuwa zikilipa kwa wakati fedha za pango, ambapo uaminifu huo utawasaidia kupata nafasi katika jengo jipya la la tatu la abiria, ambalo litakuwa linauwezo wa kuhudumia abiria milioni sita (6) kwa mwaka.
Pia amewataka wale wasiowaaminifu wachague kulipa madeni ya pango au wanaodaiwa na serikali au kuondoka, ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengine ambao wanania ya dhati ya kufanya biashara na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wasimamizi wakuu wa viwanja vya serikali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alisema tayari zabuni mbalimbali zimeshatangazwa na kuwataka wadau waliowaaminifu kujitokeza kuwania na kupata nafasi ya kufanya shughuli zao kwenye eneo la JNIA.
“Tumeshatangaza zabuni hizo na kama mhe. Waziri alivyosema zitakuwa za uwazi zikishirikisha wataalamu na tunauhakika watapatikana watu wenye mapenzi mema ya kufanya biashara na serikali” alisema Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) na kuridhishwa na kasi ya ujenzi, ambapo amewapongeza TAA, Tanroads na Kampuni ya ujenzi ya Kimataifa ya Uholanzi (BAM).
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Mayongela, alisema kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa nyingi za biashara zikiwemo uwekezaji katika hoteli, kumbi za mikutano, ofisi, migahawa, maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali, huduma za kifedha (benki) na karakana za ndege.Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (katikati mbele) akiwa katika chumba cha mikutano cha Kampuni ya ujenzi ya Kimataifa ya Uholanzi (BAM) linalojenga Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) alipofanya ziara. (Wa kwanza kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela na (wa kulia) ni Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni