Timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' leo Jumatatu inakamilisha hatua ya makundi ikicheza mchezo wake wa mwisho wa kundi 'A' dhidi ya wenyeji Harambee Stars ya Kenya utakaofanyika Uwanja wa Kenyatta, Machakos.
Mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni unachukuliwa kwa uzito mkubwa na Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje ambaye amesema hataki kuondoka Kenya na pointi moja pekee bali angalau washinde na kupata pointi nne.
Amesema wengi wanauchukulia mchezo huo ni kama wa kukamilisha ratiba, lakini kwao wanaingia kwa nia ya kushinda kwa sababu ni mechi ya ushindani na kila anayecheza anahitaji kushinda.
“Pamoja na kwamba tumeshatolewa na wengi wanachukulia kesho ni kukamilisha ratiba, sisi tunakwenda kwenye mchezo wa kesho kwa nia ya ushindi kwa sababu tunataka tutoke angalau na pointi zaidi ya hiyo moja tuliyokuwa nayo kwa hiyo tutaingia kupambana kupata ushindi,” amesema Ninje.
Kilimanjaro Stars itaendelea kuwakosa beki wa kati Kelvin Yondan ambaye bado ana maumivu ya kifundo cha mguu na Mbaraka Yusuph aliyepata majeraha ya misuli.
Kilimanjaro Stars ipo mkiani mwa Kundi A wakiwa na pointi moja waliyoipata kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Libya ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.Zanzibar wanaongoza kundi hilo A wakiwa na pointi saba wakifuatiwa na Kenya wenye pointi tano, Rwanda wenyewe wana pointi nne wakati Libya wana pointi tatu.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni