Baada ya droo ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup - ASFC), kukamilika Jumatano Desemba 06, 2017 kwenye Studio za Kituo cha Televisheni cha Azam, kilichopo Tabata relini, Dar es Salaam, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa ratiba rasmi ya mechi hizo za raundi ya pili.
Kwa mujibu wa TFF, michuano hiyo imepangwa kucheza kwa siku tano ambazo ni Desemba 20, 21, 22, 23 na 24. Mchezo kati ya Simba na Green Warriors utaochezwa Desemba 22, utakuwa ni maalumu kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa michuano hiyo msimu. Sababu Simba ndiye bingwa mtetezi.
Ratiba hiyo iliyotolewa leo Desemba 12, 2017 inaonesha michezo ya Desemba 20, mwaka huu itakutanisha timu za JKT Mlale na KMC; Toto African ya Mwanza na Eleven Stars ya Kagera; Ambassador na JKT Oljoro; Boma FC na Ndanda; Mvuvumwa na JKT Ruvu; Abajalo itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons wakati Milambo ya Tabora itacheza Buseresere ya Geita.
Desemba 21, 2017 Mshikamano itacheza na Polisi Tanzania; Rhino ya Tabora na Alliance ya Mwanza; Majimaji Rangeres ya Lindi itapambana na Mbeya Kwanza ya Mbeya; Njombe Mji na Mji Mkuu ya Dodoma; Ashanti na Friends Rangers za Dar es Salaam; Kagera Sugar na Makambako wakati Stand United ya Shinyanga itacheza na AFC ya Arusha.
Desemba 22, mwaka huu kutakuwa na mechi za Green Warriors na Simba; Polisi Dar itapambana na Mgambo JKT ya Tanga; Kariakoo ya Lindi na Transit Camp ya Dar ila kwa sasa imeweka maskani Shinyanga; Biashara ya Mara itacheza na Mawenzi Market ya Morogoro; Ruvu Shooting ya Mlandizi mkoani Pwani itacheza na Madini FC ya jijini Arusha huku Mufindi United na Pamba ya Mwanza ilihali Singida United itacheza na Bodaboda FC.
Siku ya Desemba 23, mwaka huu Azam FC itacheza na Area C; African Lyon ya Dar es Salaam na Kiluvya United ya Pwani; Makanyagio itapambana na Mbao; Mwadui na Pepsi; Majimaji na New Generation wakati Mbeya City itacheza na Ihefu.
Desemba 24, 2017 Young Africans itacheza na Reha FC; Burkina ya Morogoro na Lipuli ya Iringa; Coastal Union ya Tanga na Dodoma Fc ya Dodoma; Shupavu na Real Mojamoja wakati Villa Squad itacheza na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni