Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesimamisha shughuli za uvuvi katika ziwa Rukwa hadi hapo wataalamu wa afya watakapojiridhisha kuwa hakuna ugonjwa wa kipindupindu katika kambi za uvuvi zinazozunguka ziwa hilo na Mkoa kwa jumla.
Amesema kuwa athari inayopatikana katika kambi hizo za uvuvi zitawaathiri wala samaki unaotokana na uvuvi wa ziwa hilowaliopo na kuongeza kuwa wale wote wanaovua samaki waliopiga kambi katikakati ya ziwa waache kuvua mara moja na wasiruhusiwe kuingia katika ili kuweza kuudhibiti ugonjwa huo.
“Kuanzia leo tunapiga marufuku shughuli zote za uvuvi, mpaka tutakapojiridhisha kwamba tuna mazingira safi na salama, na kwamba maisha yetu hayapo hatarini tena na hao mnaosema wanakuja hawatapata maeneo ya kuuzia samaki wao tena watatafuta pa kwenda na tutaweka kambi ya kudhibiti wagonjwa wanaotoka huko wataishia hapa hawatakwenda popote,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo alipofanya ziara katika kambi ya mererani iliyopo katika kijiji cha Ilanga, Kata ya Muze Wilaya ya Sumbawanga katika bonde la Ziwa Rukwa ambapo mpaka anafiak hapo palikuwa na wagonjwa 9 wa kipindupindu.
Awali akitoa taarifa ya ugonjwa huo Afisa afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Plasidus Malapwa ameeleza kuwa ugonjwa huo ulibainika tarehe 23/11/2017 kutokana na mgonjwa aliyetoka kambi ya Lichili, Kijiji cha Lichili, Wilaya ya Momba, Mkoani Songwe na kufia katika kambi ya kamchanga, Kata ya Muze, wilayani Sumbawanga na wagonjwa kuanza kuongezeka hali iliyosababisha kuanzisha kambi nne kuzunguka ziwa Rukwa.
“hali ya Wagonjwa toka tarehe 1/12/2017 hadi hivi sasa katika kambi nne ni kama ifuatavyo; Muze wagonjwa 4 wameongezeka leo wawili wapo 6 hakuna kifo, Kipa wagonjwa 8, vifo 2, kamchanga wagonjwa 26, vifo 3, matete wagonjwa 6, hakuna kifo hivyo jumla ya wagonjwa wote tangua kuanza kwa mwezi wa 12 ni waginjwa 46 na vifo 5,” Aliorodhesha.
Nae Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Muze aliongeza kuwa, kuna hatua mbalimbali zilizochukuliwa ili kudhibiti ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kufungia migahawa michafu 8 hadi watakapotekeleza maelekezo ya wataalamu wa afya, pombe mapipa 4 na debe 3 ilimwagwa na wanywaji pombe 14 walilipishwa faini ya shilingi 20,000/= kila mmoja.
Tangu ugonjwa huo uanze tarehe 20/11/2017 hadi 13/12/2017 kuna wameripotiwa wagonjwa 52 na vifo 6.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni