Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima ya Taifa Tanzania { NIC } Nd. Sam Kamanga Kulia akimkabidhi Hundi ya Shilingi Milioni 20,000,000/- Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi inayotokana na mchango aliokuwa akichangia Bima ya Pencheni tokea Mwaka 2009.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima ya Taifa Tanzania { NIC } Nd. Sam Kamanga akifafanua jambo wakati wa mafunzo mafupi waliyopatiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya umuhimu wa kuweka Bima.
Kulia ya Nd. Sam Kamanga ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Kushoto ya Nd. Sam ni Meneja wa Bima za M,atibabu Nd. Henry Mwaliswi.
Balozi Seif Ali Iddi akitoa shukrani zake baada ya kukabidhiwa Hundi ya Shilingi Milioni 20,000,000/- inayotokana na mchango aliokuwa akichangia Bima ya Pencheni tokea Mwaka 2009. Picha na – OMPR – ZNZ.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima ya Taifa Tanzania { NIC } Nd. Sam Kamanga ameikumbusha Jamii ya Watanzania kujenga Utamaduni wa Kujiwekea Bima kulingana na Mazingira wanayoishi au kufanyia kazi ili iwe faraja wakati wanapokumbwa na Majanga.
Alisema Watu wote wanaelewa thamani na umuhimu wa Fedha ambayo inakuwa na mazingira ya utata katika matumizi yake iwapo hakutakuwa na maandalizi mazuri hasa katika kujiwekea hakiba kwa ajili ya matukio ya dharura.
Ndugu Sam Kamanga alisema hayo katika hafla fupi ya kumkabidhi Hundi ya Shilingi Milioni 20,000,000/- Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi inayotokana na mchango aliokuwa akichangia wa Bima ya Pencheni tokea Mwaka 2009.
Hafla hiyo fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa juu wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar iliambatana pia na mafunzo mafupi yaliyotolewa na Wataalamu wa Shirika hilo la Bima ya Taifa Tanzania kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Nd. Sam Kamanga alisema Mwanajamii anapoamua kujiwekea mpango wa utaratibu wa kuwa na Bima kwa mujibu wa mazingira yake huiwezesha Jamii yake kuwa na kinga inayowawezesha kuondokana na machungu ya majanga.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Shirika la Bima ya Taifa Tanzania { NIC } aliwanasihi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutumia Bima ya Vikundi kwa mujibu wa Utumishi wao wa Miaka Mitano ambao unaweza kuwasaidia wakati wanapomaliza Utumishi wao kwa Wananchi.
Akipokea Hundi ya Shilingi Milioni 20,000,000/- kutokana na Mchango wake wa Miaka Kumi kwenye Bima ya Pencheni katika Shirika la Bima ya Taifa Tanzania { NIC } akiwa Mbunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Balozi Seif alilishukuru Shirika hilo kwa ushawishi wake uliopelekea kuwa Mwanachama wao.
Balozi Seif ambae ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa Shirika hilo kuendelea kutoa Elimu ya umuhimu wa Mwana Jamii kujiwekea Bima Mjini na Vijijini Tanzania Bara na Zanzibar ambayo husaidia kutuliza amani ya moyo ya mteja na Familia yake.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na kupokea Hundi hiyo kulingana na mchango wake tokea alipoamuwa kujisajili kuwa Mwanachama wa Shirika hilo kupitia Bima ya Pencheni ambayo hulipwa Mteja anapomaliza muda wake wa Utumishi.
Mapema wakitoa Mada Mkurugenzi wa Bima za Maisha Bwana Michael Moe na Meneja Bima za Maisha wa Shirika la Bima ya Taifa Tanzania { NIC } Ishaka Kibamba walisema ni vyema kwa Waajiriwa wa Mikataba ya Muda Mfupi wakajifungulia Bima kwa lengo la kujiandaa na maisha yao ya baadaye.
Walisema hatua hiyo inalenga kupunguza msongo wa Kimaisha ambao huonekana kuwazonga Watu wengi wakiwemo pia Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wanapomaliza utumishi wao bila ya kujiwekea hatma njema.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/12/2017.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni