Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa
Taasisi ya Uhasibu Tanzania Wakili Said Chiguma akielezea weledi wa
wahitimu wa Chuo hicho unaosababisha wengi kupata taaluma ya juu ya
Uhasibu- CPA wakati wa Mahafali ya 15 ya Chuo hicho kwa Kampasi ya
Mtwara na Dar es Salaam, yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na wahitimu wa Kozi
mbalimbali katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania – TIA kuhusu
kujiepusha na masuala ya Rushwa wawapo kazini wakati wa Mahafali ya
15 ya Chuo hicho kwa Kampasi ya Mtwara na Dar es Salaam, Jijini Dar
es Salaam.
Baadhi ya Wahitimu wa Kozi
mbalimbali wa katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania-TIA Kampasi ya Dar
es Salaam na Mtwara, wakisubiri kwa hamu kutunukiwa shahada zao
katika Mahafali ya 15 ya Chuo hicho kwa Kampasi ya Mtwara na Dar es
Salaam, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ( kushoto) akimpa zawadi Bw. Fransis
Levis Mwanafunzi aliyefanya vizuri katika masomo yake katika Taasisi
ya Uhasibu Tanzania (TIA), Jijini Dar es Salaam.
Wahitimu wa Shahada ya Kwanza katika
Taasisi ya Uhasibu Tanzania – TIA wakiwa na furaha baada ya
kutunukiwa vyeti vya Kozi mbalimbali na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) Jijini Dar es
Salaam.
Na. Benny Mwaipaja
Na. Benny Mwaipaja
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mhe
Dkt. Ashatu Kijaji, amewataka wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu
Tanzania (TIA) kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilrifu wawapo
kazini na badala yake wafanye kazi kwa bidii, uadilifu, umakini kwa
kuzingatia Sera, sheria, kanuni na taratibu za kitaaluma
zilizowekwa.
Dkt. Kijaji aliyasema hayo wakati
akiwatunuku vyeti vya kozi mbalimbali wahitimu 3,538 wa Taasisi ya
Uhasibu Tanzania- TIA, wakati wa mahafali ya 15 ya Chuo hicho kwa
Kampasi ya Dar es Salaam na Mtwara, Jijini Dar es Salaam.
‘Vitendo vya rushwa na ubadhirifu
vina madhara makubwa kwa maisha ya mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa
letu kwa ujumla, ni vyema kila wakati mkumbuke kuwa rushwa ni adui wa
haki na maendeleo ya Taifa.’ Alieleza Dkt. Kijaji.
Aliwataka Wahitimu wa Taasisi hiyo
kujielekeza katika kujiajiri na kuajiri wengine kutokana Soko dogo la
ajira hasa ajira rasmi ambalo halikidhi mahitaji ya wahitimu wote
nchini.
‘Hatua mliyofikia iwe chachu ya
kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la
ajira na kujiajiri bila kufanya hivyo kazi nyingi za ndani
zitachukuliwa na wageni kutoka nje’, alisisitiza Naibu Waziri
Kijaji.
Alisema kuwa TIA ni miongoni mwa
Taasisi za Elimu ya Juu nchini zinazotoa mafunzo kwa viwango vya
kimataifa hivyo ni vyema kuendeleza mafanikio yaliyopatikana bila
kusahau kuboresha mahali palipo na mapungufu.
Dkt. Kijaji alisema kuwa fani za
Uhasibu ikiwemo Uhasibu wa Fedha za Umma, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi
wa Biashara, Uongozi wa Raslimali Watu na Masoko ni muhimu katika
kuendesha uchumi wa viwanda, hivyo umahiri wa wataalamu wanaozalishwa
katika taasisi hiyo unatakiwa kuonekana katika kukabiliana na
changamoto za usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma,
mahitaji ya Soko, ushindani na utandawazi.
Taasisi ya TIA imetakiwa kuendelea
kuboresha mitaala ili kukidhi viwango vya kimataifa kwa kuwa Dunia ya
sasa ni ya teknolojia hivyo kama Taasisi inatakiwa kuendana na
teknolojia hiyo ambayo itasaidia kubadilishana maarifa.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu
wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Dkt. Joseph Kihanda alisema kuwa
kati ya wahitimu 3,538 wanawake ni 1,846 sawa na asilimia 52.2 na
wanaume ni 1,692 sawa na asilimia 47.8. Wahitimu 233 ni wa Kampasi ya
Mtwara na wahitimu 3,305 ni wa Kampasi ya Dar es Salaam.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri
wa Taasisi hiyo Wakili Said Musendo Chiguma alisema kuwa kwa miaka
miwili mfululizo kuanzia mwaka 2015/2016 na 2016/2017 Taasisi hiyo
imeongoza kwa kutoa wafaulu wengi wa shahada za juu ya taaluma ya
Uhasibu- CPA na taaluma ya Ugavi- CPSP ambapo kwa kipindi cha miaka
mitano imetoa asilimia 10 ya wahitimu wote kitaifa.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Ashatu Kijaji amewapongeza Wahitimu wote kwa jitihada
walizozifanya hadi kufikia hatua hiyo ya kupata vyeti japokuwa
amewahimiza kujiendeleza zaidi kitaaluma ili kuongeza weledi.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
15 Desemba 2017
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni