KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, ameongoza waombolezaji na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo kumzika Katibu Mkuu Mstaafu na Mlipaji Mkuu wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, Marehemu Ramadhani Mussa Khijjah, aliyefariki jana alfajiri nyumbani kwake Jet Lumo, Wilayani Temeke, Jijini Dar es Salaam, akiwa na umri wa miaka 65.
Marehemu Khijjah amezikwa katika Makaburi ya Kisutu Jijini Dar es Salaam, saa 10 jioni, na maziko yake yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, na dini, halkadhalika na baadhi ya Makatibu Wakuu Wastaafu.
Akielezea wasifu wa marehemu Khijjah, katika risala iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa ununuzi wa Umma wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Iddi Lemmah, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James ameelezea masikitiko yake kufuatia kifo hicho na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Marehemu Ramadhani Mussa Khijjah aliajiriwa na Wizara ya Fedha tarehe 06 Aprili, 1976 kwa cheo cha Mtakwimu Daraja la III na akapandishwa cheo Mnamo tarehe 01 Agosti, 1979 kuwa Mtakwimu Daraja la II, na tarehe 01 Aprili, 1981 alibadilishwa Kada kuwa Mchumi Daraja la II.
"Kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi pamoja na uadilifu aliendelea kupandishwa cheo kuwa Mchumi Mwandamizi Daraja la I na tarehe 1 Februari, 1988 alipandishwa cheo kuwa Mchumi Mwandamizi Daraja la III. Wizara iliendelea kumpandisha vyeo ambapo tarehe 01 Agosti, 1991 alipandishwa cheo kuwa Mchumi Mwandamizi Daraja la II" ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo
Mnamo tarehe 26 Januari, 1993 aliteuliwa kuwa Kamishna wa Sera na Utafiti, cheo ambacho aliendelea kukitumikia hadi alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo ya Fedha tarehe 28 Novemba, 2002.
Tarehe 23 Novemba, 2008 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali nafasi ambayo aliitumikia hadi alipostaafu kwenye Utumishi wa Umma mnamo tarehe 11 Juni, 2013.
Marehemu Ramadhani Mussa Khijjah alikuwa mchapakazi mwadilifu katika utumishi wake na hii imedhihirisha wazi ambapo mnamo tarehe 09 Desemba, 2012 katika Maadhimisho ya Sherehe ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Mheshimiwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alimtunuku nishani ya Utumishi mrefu na maadili mema katika Utumishi wa Umma.
"Kwa masikitiko makubwa Viongozi na Wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango tunaungana na familia ya marehemu katika maombolezo ya msiba huu mkubwa na tunaahidi kuenzi hazina aliyotuachia" alieleza Bw. Iddi Lemmah.
Imetolewa na
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni