WAKATI Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Bi. Easter Kazenga amezipongeza timu za sekta hiyo kwa kufanya vyema kwenye mashindano ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Iringa, leo kwenye uwanja wa Samora timu ya soka iliwachapa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa bao 1-0.
Bi. Kazenga amezipongeza timu za michezo ya kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume, soka, netiboli, karata, bao, draft, riadha na baiskeli za Uchukuzi baada ya kuwatembelea kwenye kambi yao mara baada ya kumalizika kwa michezo.
“Ninawapongezeni sana kwa kufanya vizuri katika michezo hii, nimekuja kuungana nanyi ili kuwatia moyo na nitakuwa hapa kwa siku kadhaa na baadaye Katibu Mkuu na wengine watakuja, hivyo tuendeleze ushindi na tuchukue vikombe vyote vya ubingwa,” amesema Bi. Kazenga.
Hatahivyo, amewasisitizia wachezaji hao kuwa na nidhamu wawapo ndani na nje ya kiwanja ili kujenga sifa nzuri ya sekta hiyo.
Uchukuzi SC inayoundwa na wachezaji wazoefu akiwemo aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Eliutely Mholeli alipata bao lake pekee kwa njia ya penati iliyofungwa na Mahamudu Khamis katika dakika ya 52 baada ya Sigfrid Kikoti kuchezewa rafu na Joseph Mlimi wa TRA.
Hatahivyo, wachezaji wa pande zote mbili walishindwa kuonesha mchezo mzuri kutokana na kucheza huku mvua ikinyesha na uwanja kujaa maji katika baadhi ya sehemu na kusababisha wachezaji kuanguka hovyo huku mpira ukikwama katika madimbwi.
Katika mchezo wa netiboli uliochezwa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUKU), timu ya Uchukuzi iliwaadhibu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwafunga magoli 38-13.
Uchukuzi SC inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa na Bandari, Judith Ilunda ilikwenda mapumziko wakiwa na magoli 15-7, ambapo hadi mwisho wa mchezo mfungaji wake Matalena Mhagama alifunga magoli 28 na Bahati Herman magoli 10, wakati wa Tanesco Tina Mbuisa magoli tisa na Caltace Manapo magoli manne.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya Msingi Mlandege, mabingwa watetezi timu ya Uchukuzi iliwavuta Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa mivuto 2-0.
Kwa upande wa wanaume mabingwa watetezi Uchukuzi waliwapeleka puta Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwavuta mivuto 2-0.
Michuano hiyo itaendelea leo kwa mechi za soka kati ya NAO dhidi ya GGM, wakati katika netiboli watacheza RAS Iringa na Hifadhi ya Ngorongoro. Mshambuliaji Ramadhani Madebe wa timu ya Uchukuzi (kulia) akikokota mpira kuelekea kwenye lango la timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakati kipa Frank Mvula na mlinzi wake Joseph Mlimi wakiwa tayari kuondoa hatari katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye leo uwanja wa Samora, ambapo TRA walichapwa bao 1-0. (Picha na Bahati Mollel-TAA)
Winga Omari Kitambo (5) wa Uchukuzi akizongwa na beki Joseph Mlimi (2) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mchezo wa michuao ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye leo uwanja wa Samora mkoani Iringa. Uchukuzi walishinda bao 1-0. (Picha na Bahati Mollel-TAA).
Kipa Frank Mvula wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akiwa ameshindwa kucheza mpira wa penati uliopigwa na Mahamudu Khamis wa Uchukuzi katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana leo uwanja wa Samora. Uchukuzi walishinda bao 1-0. (Picha na Bahati Mollel-TAA).
Timu ya wanawake na kamba ya Uchukuzi wakiwavuta Tanesco (hawapo pichani) katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege. Uchukuzi ambao ni mabingwa watetezi wameshinda kwa mivuto 2-0. (Picha na Bahati Mollel-TAA).
Mchezaji wa timu ya wanawake ya Tanesco, Tina Mbusa akiongoza jahazi la Tanesco katika mchezo wa kuvuta kamba dhidi ya Uchukuzi, uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Mlandege. Uchukuzi walishinda kwa kuvuta mivuto 2-0. (Picha na Bahati Mollel-TAA)
Timu ya Wanaume ya Uchukuzi (kulia) wakiwavuta TRA katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege. Uchukuzi ambao ni mabingwa watetezi walivuta mivuto 2-0. (Picha na Bahati Mollel-TAA).
Winga Pendo Rungu wa Tanesco (WA) akidaka mpira uliorushwa na Shaila Mhava (C) huku Neema Makassy (WD) na Subira Jumanne (C-jezi nyeusi) wa Uchukuzi wakijiandaa kuokoa hatari iliyokuwa ikielekezwa kwenye lango lao katika mchezo wa Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUKU) Iringa. (PIcha na Bahati Mollel-TAA)
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Bi Easter Kazenga (aliyevaa suti ya michezo rangi ya kijivu katikati mbele), leo akiwa na kikosi cha wachezaji wa michezo mbalimbali ya timu ya Uchukuzi inayoshiriki katika michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika mkoani Iringa. (Picha na Bahati Mollel-TAA).
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni