.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 29 Januari 2014

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YATOA MAFUNZO KWA WADADISI NA WAHARIRI WA MADODOSO YA UTAFITI WA WATU WENYE UWEZO WA KUFANYA KAZI KWA MWAKA 2014


PICHA 1Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akitoa maelezo ya utangulizi ya kufungua mafunzo ya Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Bene uliopo Morogoro mjini.
Mkuu wa Mkoa wa Mororgoro Mhe. Joel Bendera akihutubia wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Bene uliopo Morogoro mjini.
Kaimu Meneja wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akitoa neno la shukrani mara baada ya hotuba ya Mgeni rasmi Mhe. Joel Bendera (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Bene uliopo Morogoro mjini.
Baadhi ya Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Bene uliopo Morogoro mjini.

Na Veronica Kazimoto – Morogoro
28 Januari, 2014

Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi popote pale duniani ni kigezo muhimu sana kinachotumika katika kupima na kufuatilia mwenendo wa mabadiliko yanayotokea katika soko la ajira ili kuiwezesha Serikali husika kuboresha Sera na Program mbalimbali za kukuza ajira nchini.
 

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera wakati akifungua mafunzo ya Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 yaliyofanyika katika ukumbi wa Bene mjini Morogoro.

 

“Utafiti huu mbali na kusaidia kufuatilia mwenendo wa soko la ajira nchini, husaidia pia kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo kama vile Malengo ya Millennia, Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 na Malengo ya MKUKUTA”, amesema Bendera.
 

Bendera amefafanua kuwa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi utatoa viashiria kama vile hali ya ajira nchini katika sekta rasmi na isiyo rasmi, kiwango cha ukosefu wa ajira, kiwango cha ajira isiyo timilifu na ajira mbaya ambayo ni hatarishi kwa watoto.
 

Viashiria vingine ni wigo wa hifadhi ya jamii na hali ya kipato kutokana na ajira, matumizi ya muda na ajira mpya zilizozalishwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2013.
 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifu ya Takwimu, amesema taarifa za hali ya soko la ajira zinazotumika kwa sasa bado ni zile za mwaka 2006.

“Takwimu za ajira zinazotumika sasa hazioneshi hali halisi ya mabadiliko yaliyotokea katika soko la ajira nchini, kutokana na hali hii Serikali pamoja na wadau wa maendeleo wameamua kufanya utafiti huu mwaka 2014 ili kupata hali halisi ya sasa”, amesisitiza Kwesigabo.
 

Jumla ya wadadisi na Wahariri 100 wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kutoka kanda ya Pwani na Kusini inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mtwara na Lindi wanaendelea kupewa mafunzo juu ya Utafiti huo utakaoanza rasmi mwezi Februari hadi Disemba mwaka huu.
 

Mafunzo kama haya yanafanyika katika kanda ya Ziwa, kanda ya Kati, kanda ya Kasikazini na kanda ya Juu Kusini ambapo ufunguzi rasmi umefanyika jana kwa baadhi ya kanda na leo katika maeneo mengine.
 

Mafunzo haya ya Wadadisi na Wahariri wa madodoso ya Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 yanafanyika mara baada ya kukamilika kwa mafunzo ya Wakufunzi wa utafiti huo takribani wiki tatu zilizopita.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni