WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaonya
Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za
uongozi na hasa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba,
2015.
Ametoa onyo hilo leo mchana
(Jumapili, Julai 27, 2014) wakati akizungumza na mamia ya waumini na
viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya
ya Ruvuma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na
kuwekwa wakfu Askofu Amon Mwenda aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo.
“Ninawasihi wananchi wawe makini
na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha
kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza
ni kwa nini atumie fedha ili kupata nafasi ya uongozi?,” alihoji.
“Tatizo ni kwamba hata wananchi
hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na wagombea. Atakuja
huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue akiingia
madarakani anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia,” alisema.
Aliwaonya wananchi kuwa makini ili
wasije wakageuzwa mtaji wa kuwanufaisha watu binafsi. “Tukikubali
kutumika ni sawa tutapata viongozi wakati wa uchaguzi, lakini
watakuwa ni wale wasio na hofu ya Mungu, wenye kujali maslahi yao
kuliko ya wananchi waliowachagua,” aliongeza.
Aliwaomba viongozi wote wa dini
waliohudhuria sherehe hizo pamoja na waumini wote waendelee kuliombea
Taifa ili Mungu aliepushe na janga hilo la watu kupenda rushwa.
Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea mchakato wa kupata
Katiba mpya ili wabunge wote warejee ndani ya Bunge na kuikamilisha
kazi waliyoianza.
Alimuomba Askofu huyo mpya apokee
jukumu hilo kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa kama Serikali
watakuwa naye bega kwa bega kuwaongoza Watanzania walioko kwenye
dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mkoa wote wa Ruvuma na
wilaya ya Ludewa eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 72,630.
Kati ya hizo km. za mraba 64,233 ni za mkoa wa Ruvuma na km. za mraba
8,397 ni za wilaya ya Ludewa.
Mapema, akitoa hotuba yake ya kwanza
mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda alisema dayosisi mpya ya
Ruvuma imezaliwa katika kipindi chenye changamoto nyingi za kidunia
na utandawazi ukiwemo mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Hata hivyo, akiainisha malengo ya
dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa kwanza, Askofu Mwenda
alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu, dayosisi hiyo itahimiza
ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya chakula cha kutosha.
Alisema watashirikiana na Serikali
na wadau wa ndani najje katika kutoa huduma za kijamii hasa elimu na
afya. Aidha alisema atakabiliana na changamoto za sasa ambazo
alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino,
unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini
wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa alisema Kanisa
lingependa kupata viongozi ambao ni wacha Mungu.
Akirejea mahubiri yake, Askofu
Malasusa alisema inashangaza kuona kuna baadhi ya watu wanagombea
nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na Mungu aliyewaumba watu
anaotaka kuwaongoza.
“Bila kujali imani ya mtu,
tunatamani tungepata kiongozi ambaye anamcha Mungu. Awe anapenda
kuhudhuria ibada. Awe anampenda Mungu ndipo atawapenda watu
anaowaongoza,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 27, 2014
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni