Kiingilio cha chini kwenye mechi ya
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba itakayochezwa
Jumamosi (Oktoba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh.
7,000.
Washabiki watakaolipa kiingilio
hicho ni wale watakaokaa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo
jumla yake ni 36,693 katika uwanja huo wenye viti 57,558. Viingilio
vingine ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa
VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Tiketi zitakazotumika kwenye mechi
hiyo ni za elektroniki, na zimeanza kuuzwa jana (Oktoba 13 mwaka
huu). Tiketi zinapatikana kwa mtandao wa M-PESA, CRDB Simbanking na
maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo zaidi ya mia moja sehemu
mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo namba 27 itakayochezeshwa
na mwamuzi Israel Mujuni Nkongo akisaidiwa na John Kanyenye na
Ferdinand Chacha itaanza saa 10 kamili jioni. Kamishna wa mechi hiyo
ni Salum Kikwamba kutoka mkoani Kilimanjaro.
Washabiki wanatakiwa kununua tiketi
mapema, kwani hazitauzwa uwanjani siku ya mechi. Milango yote ukiwemo
ule wa upande wa Mbagala (Uwanja wa Ndani) itafunguliwa kwa ajili ya
washabiki, na itakuwa wazi kuanzia saa 4 asubuhi.
Magari maalumu tu yenye stika ndiyo
yatakayoruhusiwa kuingia uwanjani kwa kupitia Barabara ya Mandela.
Pia washabiki hawaruhusiwi kuingia uwanjani wakiwa na silaha, vitu
vya vyuma na mabegi makubwa. Barabara ya kuingilia upande wa
Chang’ombe itafungwa kwa watumiaji wa magari.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA
MIGUU TANZANIA (TFF)

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni