IGP Ernest Mangu
Na, Mwandishi wetu
Kiongozi wa watuhumiwa urushaji
mabomu nchini na umwagaji tindikali, Yahaya Hassan Omari Hela maarufu
kwa jina la Yahaya Sensei (31) mkazi wa Mianzini Jijini Arusha,
amefariki dunia usiku wa kuamkia leo,baada ya kupigwa risasi na
Polisi eneo la mguu na tako la kulia, wakati alipojaribu kuruka ndani
ya gari la Polisi kwa lengo la kutoroka.
Akizungumza leo na waandishi wa
habari Jijini Arusha, kamanda wa Polisi, Liberatusi Sabas, amesema
polisi walimuua Oktoba 19 mwaka huu majira ya saa 5:30 Usiku huko
eneo la Kisongo, Wilayani Monduli, katika barabara ya Arusha-Babati,
wakati wakielekea kijijini kwake, alikozaliwa Chemchem Wilayani
Kondoa, Mkoani Dodoma kwa lengo la kwenda kuonyesha bomu lililoko
huko.
Amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa
mwalimu wa Karate na Judo na alikuwa muasisi na kinara wa matukio ya
ugaidi yaliojitokeza Jijini Arusha, Zanzibar, Mwanza na Dar es
Salaam.
Sabas amesema kupatikana kwa
marehemu huyo kumetokana na Intelejensia imara ya Polisi ya kisasa na
ya hali ya juu na walimkamata Mkoani Morogoro Oktoba 6 mwaka huu,na
kusafirishwa Oktoba 11 mwaka huu kuletwa Jijini Arusha, na
alipohojiwa alikiri kuhusika na kuratibu matukio mbalimbali ya ugaidi
na alikuwa kijificha kwenye nyumba tofauti na porini.
Amesema kuwa Mtuhumiwa huyo alipigwa
risasi kwenye mguu wa kulia na kalio la kulia pale alipojifanya
kutumia uzoefu wake wa Judo na Karate na alipokimbizwa Hospitali ya
Mkoa kwa matibabu alifariki njiani na mwili wake umehifadhiwa kwenye
chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo.
Sabas amesema baada ya kumkamata
ametaja baadhi ya matukio tisa aliyoshiriki kufanya ya umwagaji
tindikali kwa baadhi ya watu na urushwaji wa mabomu maeneo mbalimbali
likiwemo la Mei 5 mwaka 2013 saa 10:30 maeneo ya Kanisa la Roman
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo Olasiti Jijini
Arusha, ambapo aliratibu kurushwa kwa bomu na kusababisha vifo vya
watu watatu na majeruhi 56.
Hata hivyo Kamanda alisema bado
wataendelea kuwakamata wengine wadogo wadogo waliopo katika kikundi
hicho ambao amewataja na amesema marehemu amekiri kuendesha Karate na
Judo kwenye baadhi ya Misikiti Jijini Arusha, ila kwa sasa hakuna
tena kazi hiyo kutokana na Polisi kusambaratisha kikosi chote.
Mwisho
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni