Shirika la Ndege la Taifa la Shelisheli, Air Seychelles
limeanza kufanya safari zake kati ya mji mkuu wa nchi hiyo, Mahe na Dar es
Salaam ambapo leo, Desemba 2, 2014, ndege yake ya abiria HM 777 ilifanya safari
yake ya kwanza ya uzinduzi kwa kutua Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Uzinduzi wa safari za ndege ya Air Seych elles ulifanywa na
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhandisi Dk. Charles Tizeba na kuhudhuriwa na Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, wabunge na viongozi kadhaa wa
Serikali na wadau wa masuala ya sekta ya usafiri wa anga na maliasili na utalii
nchini.
Katika hotuba yake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhandisi Dk.
Tizeba alisema ujio wa Air Seychelles umefungua ukurasa mpya wa safari kwa
wananchi wa nchi za zisizopakana na bahari ya Hindi (landlocked) na fursa zaidi
za utalii kwani sasa watakuwa na uhakika wa kuunganisha safari zao kwenda
kokote duniani kwa ndege hiyo.
Naibu Waziri Tizeba alisema ujio wa ndege hiyo utakuza sekta
ya utalii kati ya nchi hizo na kunufaisha wananchi wake na kwa kujua umuhimu wa
sekta ya usafiri wa anga kwa nchi hizo, alizitaka Tanzania na Shelisheli
kutekeleza mikakati ya kitaifa, kikanda na dunia ya usafiri wa anga kuleta
maendeleo ya sekta hiyo nchi mwao.
Alitoa rai kwa wafanyabiashara ya sekta ya utalii kutumia
fursa hii kukukuza biashara kati ya nchi hizi kwani Tanzania ina hazina ya
vivutio vya utalii ikiwemo maeneo ya kihistoria Zanzibar na Bagamoyo, mlima
mrefu kuliko yote Afrika, Kilimanjaro na moja ya maajabu saba ya dunia, Kreta
ya Ngorongoro mkoani Manyara.
Naibu Waziri Dk. Tizeba alisema, Serikali itafanya kila
iwezalo kuhakikisha safari za ndege kati ya Tanzania na Shelisheli zinadumu na
kwamba Serikali za nchi hizo zitahakikisha mkataba wa ushirikiano wa sekta ya
usafiri unasainiwa haraka iwezekanavyo na mamlaka husika za usafiri wa anga
nchini kwa mujibu wa masharti ya ICAO.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), Mhandisi Suleiman S. Suleiman alisema ujio wa ndege hiyo ni mafanikio
makubwa kwani unaongeza idadi ya ndege zinazotua JNIA ambapo juzi tu ilikuja
Flydubai na wanatarajia mwakani, 2015 Emirates itaongeza safari kutoka 12 hadi
14 kwa wiki.
“Sisi (TAA) hatulali. Tunafanya kazi kwa ushirikiano na
mshauri mwelekezi wa biashara ya ndege ambaye kazi yake ni kushawishi mashirika
zaidi ya ndege kuja Tanzania. Mpaka sasa kuna ndege 18 zinazokuja na Januari
mwakani, 2015, ndege ya Etihad inatarajiwa kuanza safari zake pia”, Mkurugenzi
Mkuu huyo wa TAA alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Mahusiano wa
Air Seychelles, Alan Renaud alisema safari za ndege hiyo kati ya Mahe – Dar es
Salaam zitakuza utalii na biashara kati ya Tanzania na Shelisheli na kuwa
kiungo cha safari za mashirika mengine ya ndege duniani ambako abiria
wataunganisha safari zao.
“Dar es Salaam ni njia nyingine muhimu ya safari za ndege
yetu tulizoongeza na inaonesha hatua mpya ya kukua kwa shirika letu. Ikiwa na
watu zaidi ya milioni nne na ya pili kwa ukubwa ukanda wa bahari ya Hindi,
kiungo kikubwa kwenda mbuga na hifadhi maarufu za wanyama na vivutio vingine
vya utalii kama Mlima Kilimanjaro wenye theluji, Dar es Salaam ni chachu kubwa
ya utalii na biashara,” alisema Renaud katika hotuba yake.
Alisema, ujio wa ndege hiyo ni matokeo ya ushirikiano mkubwa
kati yao na Shirika kubwa la ndege la Etihad Airways lenye hisa asimia 40
lililowawezesha kupata ndege ya kwanza aina ya Airbus A320 na kuifanya Mahe
kama kitovu cha abiria kutoka Afrika Mashariki kwenda nchi za Mashariki ya
Kati, Asia na za Bara Hindi.
Air Seychelles ilianzishwa mwaka 1978 na ilianza safari za
masafa marefu mwaka 1983. Kwa sasa shirika hilo la ndege linafanya safari
kwenda Abudhabi, Antananarivo (Madagascar), Hong Kong, Johannesburg (Afrika
Kusini), Mauritius, Mumbai (India) na Paris (Ufaransa) na safari 200 za ndani
mwake kwa wiki. Air Seychellles itafanya safari zake kati ya Mahe na Dar es
Salaam (JNIA) mara mbili kwa wiki, Jumanne na Jumapili.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni