.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 18 Februari 2015

RAIS WA ZANZIBAR, DR.SHEIN ASISITIZA WATAALAM WAZALENDO WATUMIKE SERIKALINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuwatumia wataalamu wazalendo katika kazi za kitaalamu za Serikali huku akiupongeza uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kufanikisha mambo mbali mbali yenye mnasaba na utekelezaji malengo na majuku yaliyowekwa na Ofisi hiyo.

Dk. Shein aliyasema hayo katika mkutano kati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, huko Ikulu mjini Zanzibar, mkutano wenye lengo la kuangalia Utekelezaji wa Malengo ya Mpango Kazi wa Ofisi hiyo hiyo kwa robo mbili kati ya Julai hadi Disemba 2014.

Katika maelezo yake Dk. Shein, alipongeza hatua zilizochukuliwa na Ofisi hiyo katika kuhakikisha malengo yaliwekwa yanafikiwa pamoja na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa ambapo pia, alieleza umuhimu wa kuwatumia wataalamu wazalendo ambao wamesomeshwa na Serikali hii badala ya kujikita zaidi na wataalamu kutoka nje ya nchi.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo, kuusisitiza uongozi wa Wizara hiyo akiwemo Waziri na Katibu Mkuu wake kuendelea na utaratibu uliwekwa na Serikali wa kutoa taarifa kwa wananchi kwa muda uliopangwa kupitia vyombo vya habari ili kuwaeleza mafanikio yaliopatika.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi na kupata mafanikio makubwa ambayo inapaswa wananchi kupewa taarifa juu ya mambo hayo sambamba na kuelezwa changamoto zilizopo na jinsi juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha na kuendeleza huduma za kijamii na miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya maji ambayo licha ya changamoto zilizopo lakini huduma hiyo imeweza kuimarika kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Mapema akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Malengo ya Mpango Kazi wa Bajeti ya Ofisi hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame alieleza majukumu, malengo, mafanikio na changamoto zilizopo na juhudi zinzochukuliwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ndani ya Idara za Ofisi hiyo.

Katika kuhakikisha kuwa matumizi ya rasilimali za umma yanafanyika kwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji Dk. Mwinyihaji alisema kuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar imekamilisha Ukaguzi wa Hesabu katika Wizara na Mashirika ya Serikali.

Dk. Mwinyi alisema kuwa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya mwaka 2012/2013 imeonesha kuwa kuna mabadiliko makubwa katika matumizi ya fedha na rasilimali za umma.

Alisema kuwa taasisi nyingi na Idara za Serikali hivi sasa zinazingatia na kufuata taratibu za matumizi za fedha na manunuzi na uuzwaji wa mali za serikali, kuweka kumbukumbu na kufunga hesabu za mwaka kwa wakati.

“Hapa tunatoa pongezi kwako mwenyewe Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa jinsi unavyotenga muda wako kujadili ripoti za CAG na jinsi unavyowaelekeza Watendani Wakuu wanavyopaswa kusimamia Wizara na Taasisi zao’,alisema Dk. Mwinyihaji.

Aidha, Dk. Mwinyihaji alisema kuwa Serikali imepitisha Sera ya Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta ya Binafsi (PPP) ambapo miongoni mwa vipaumbele katika Sera hiyo ni kuimarisha huduma na ujenzi wa miundombinu ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.

Pamoja na hayo, Waziri Mwinyihaji alieleza kuwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali inaendelea na ukusanyaji wa taarifa za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya wa mwaka 2014/2015.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyihaji alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa niaba ya uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuimarisha ustawi wa jamii zikiwemo huduma za afya, elimu na nyenginezo hasa tamko lake la hivi karibu na kuondoa michango maskulini sambamba na tamko la kutotozwa fedha akina mama wanaofika hospitali kwa ajili ya kujifungua.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mazee alitoa pongezi kwa Ofisi hiyo kwa juhudi iliyozichukua katika uwasilishaji mzuri wa MpangoKazi wake sambamba na utekelezaji wa malengo na majukumu kwa Ofisi hiyo. Katika Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd nae alihudhuria.

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Ungozi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambapo Waziri wa anchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Fatma Alhabib Fejej alitumia fursa hiyo kueleza mambo muhimu yaliyofanikishwa na Ofisi hiyo katika katika kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka 2014 ikwia ni pamoja na kukamilisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar.

Aidha, elieleza kuwa Ofisi hiyo imeweza kuimarisha Kamati za Usimamizi wa Ukanda wa Pwani na uundaji wa Kamati mpya sita kupitia mradi wa maabara ya utalii ambapo Kamati hizo sasa zinatarajiwa ziwe na msukumo mkubwa katika kukuza na kuendeleza utalii ambao ndio tegemeo la Utalii.

Akiendelea alieleza mafanikio mengine ambayo ni kupunguza nyumba zinazotumika kufanya biashara ya dawa za kulevya katika Shehia tano za Wilaya ya Mjini, hata hivyo Waziri Ferej alisema kuwa changamoto kadhaa zimejitokeza ikiwemo wahalifu kutumia njia mpya katika kuendeleza uhalifu wao huo.

Aidha, Uongozi huo ulitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa uelewa wake mkubwa katika masuala mtambuka na jinsi na jinsi alivyoamua na kudhamiria kuyashughulikia ipasavyo.

Sambamba na hayo, Ofisi hiyo iliahii kuongeza bidii ili kuhakikisha dhamiri yake ya kuwa na jamii ya Wazanzibari yenye mazingira endelevu, buila dawa za kulevya, maambukizi zero ya vizusi vya UKIMWI, na jamii yenye kuwajumuisha watu wenye ulemavu inafikiwa.

Mapema, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd, aliupongeza uongozi huo kwa mafanikio uliyoyapata na kazi kubwa inayofanya katika kupambana na UKIMWI pamoja na suala zima la mazingira hasa katika kupambana na matumizi ya mifuko ya plastiki.

Aliongeza kuwa ipo haja kwa Ofisi hiyo kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maliasili katika kupambana na uharibifu wa mazingira hasa matumizi mabaya ya moto kwa misitu hali ambayo imekuwa ikileta athari kubwa kwa misitu hapa nchini huku akitolea mfano wa moto ulioathiri msitu wa Jozani hivi karibuni.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi huo kwa uwasilishaji wao wa Mpango Kazi wao huo mzuri huku akieleza kuvutiwa kwake na mafanikio yaliopatikana katika Mpango wa kupambana na dawa za kulevya unaofanywa na Ofisi hiyo.

Pmaoja na hayo, Dk. Shein alieleza umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi kwa kila muda uliopangwa na Serikali ili kwajue juhudi zilizofikiwa sambamba na kusisitiza haja ya kuwatumia wataalamu wazalendo katika kazi na shughuli mbali mbali za kitaalamu Serikalini badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.


Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni