Jumanne, 31 Machi 2015
DK. SHEIN AZIPONGEZA SERIKALI ZA INDIA, OMAN NA KUWAIT KWA KUIMARISHA SEKTA ZA MAENDELEO NCHINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali za Kuwait, India na Oman katika kuwaunga mkono ndugu zao wa Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ni chachu ya kuendeleza uhusianio na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na nchi hizo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar kwa nyakati tofauti wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jasem Ibrahim Al Najem, Balozi Mdogo mpya wa India aliyepo Zanzibar Mhe. Satender Kumar na Mhe. Ali Abdulla Al-Rashdi Balozi mdogo mpya wa Oman aliyepo Zanzibar.
Katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Mhe. Jasem Ibrahim Al Najem, Dk. Shein alisema kuwa Kuwait imekuwa mshirika mzuri katika kuisaidia Tanzania ikiwemo Zanzibar hatua ambayo imeianza kwa muda mrefu.
Dk. Shein alisema kuwa nchi hiyo imeweza kusaidia sekta mbali mbali zikiwemo miundombinu ya mawasialiano ya barabara, madaraja, maji safi na salama, elimu na sekta nyenginezo kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa fedha wa nchi hiyo.
Aidha, Dk. Shein alimpongeza Balozi huyo kwa kuteuliwa kuja kuifanyia kazi nchi yake hapa Tanzania na kutumia fursa hiyo kutoa shukurani zake kwa Balozi huyo kwa azma yake ya kuitangaza Zanzibar nchini mwake kupitia makampuni kadhaa ya uwekezaji.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwakaribishwa wawekezaji kutoka nchini Kuwait kuja kuekeza katika sekta mbali mbali hapa Zanzibar zikiwemo viwanda, uvuvi, utalii na nyenginezo.
Dk. Shein alimueleza Balozi Jasem Ibrahim Al Najem mafanikio yaliopatikana Zanzibar katika sekta ya utalii ambayo ndio sekta muhimu na inayochangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa sambamba na juhudi za Serikali inazozichukua katika kuiimarisha sekta hiyo ili izidi kuimarika.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo mafanikio yaliopatikana katika kuuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaofikia miaka 51 tangu kuasisiwa kwake ambao ni wa kupigiwa mfano katika bara la Afrika sambamba na kumueleza mafanikio yaliopatikana katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayoiongoza hapa Zanzibar.
Nae Balozi Al Najem alimueleza Dk. Shein jinsi nchi hiyo inavyothamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Kuwait na kusisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa jumla ili kukuza uhusiano na ushirikiano huo.
Balozi huyo alieleza kuwa Kuwait ni mshirika mzuri wa maendeleo hapa Tanzania hatua ambayo imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta za maendeleo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika maelezo yake, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa na Kuwait katika kuhakikisha wawekezaji kutoka kampuni mbali mbali za nchini humo wanafika Zanzibar kuangalia maeneo ya kuekeza.
Alisema kuwa tayari Kuwait kupitia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi hiyo wanafanya shughuli zao katika nchi za Afrika ikiwemo Kenya, Afrika Kusini na nyenginezo, hivyo kuna haja ya kuja kufanya shughuli zao kama hizo hapa Zanzibar.
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi mdogo mpya wa India anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Mhe. Satendar Kumar ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao wameahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya pande mbizi hizo.
Dk. Shein kwa upande wake aliipongeza Serikali ya India kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu, kilimo na nyenginezo.
Kwa upande wa sekta ya afya, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Zanzibar na India hasa kufuatia ziara aliyoifanya Februari, 2014 ambapo mambo kadhaa ya kimaendeleo yalijadiliwa kati yake na viongozi wa nchi hiyo ukiwemo utiaji saini kati ya Zanzibar na hospitali ya Manipal iliyopo Bangalore nchini India.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pia, alikutana na Balozi Mdogo mpya wa Oman anayefaya kazi zake hapa Zanzibar Mhe.Ali Abdulla Al Rashdi na kufanya nae mazungumzo yaliyojikita zaidi katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Zanzibar na Oman.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Oman chini ya kiongozi wake Sultan Qaboos Bin Said Al Said kwa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya kwa msaada wake mkubwa wa ujenzi wa Chuo cha Afya, hapa Zanzibar.
Balozi huyo wa Oman aliahidi kuendeleza ushirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Oman hasa katika uimarishaji wa sekta za maendeleo huku akisisitiza azma ya nchi yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar hasa katika sekta ya afya na uvuvi sambamba na kusaidia vifaa kwa ajili ya Kiwanda cha Uchapaji cha Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni