.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 6 Machi 2015

KIINGILIO CHA CHINI KUZIONA YANGA NA SIMBA SH 7,000/=

Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea mwishoni mwa wiki kwa viwanja sita kutimua vumbi, michezo mitatu ikifanyika siku ya jumamosi na michezo mingine mitatu kufanyika siku ya jumapili.

Katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wenyeji timu ya Polisi Morogoro watawakaribisha maafande wa Ruvu Shooting kutoka Mlandizi, Coastal Union watakua wenyeji wa Kagera Sugar kwenye dimba la Mkwakwani, huku JKT Ruvu wakiwakaribisha Azam FC katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Jumapili Mgambo JKT watakua wenyeji wa timu ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Mtibwa Sugar wakiwa wenyeji wa wagonga nyundo timu ya Mbeya City katika Uwanja wa Manungu Turiani.

Katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam watani wa jadi Simba SC watakuwa wenyeji wa Young Africans, mchezo unaotarajiwa kuanzakutimua vumbi majira ya saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

KUZIONA SIMBA, YANGA SH.7,000

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa siku ya jumapili kati ya Simba SC na Young African utakaofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 kamili za jioni.

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, akisaidiwa na Soud Lila (DSM) mshika kibendera wa kwanza, Florentina Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa pili, Mwamuzi wa akiba Israel Mjuni (DSM), na kamisaa wa mchezo ni Ame Santimeya (DSM).

Viingilio vya mchezo huo, VIP A sh. 40,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh. 20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya Bluu na Kijani ikiwa ni sh. 7,000.

Tiketi zitaanza kuuzwa keso (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi katika vituo vya, Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).

Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru, barabara ya Chang'ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.

TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.

Aidha katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).


TAIFA STARS KUIVAA MALAWI

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashuka dimbani jumapili Machi 29 mwaka huu, kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mchezo huo wa kirafiki ambao upo katika kalenda ya FIFA kwa timu za Taifa (Machi 23-31) na utatarajiwa kuanza majira ya saa 10 na nusu jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

NKONGO KUCHEZESHA ZESCO Vs AS KALOUM

Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania mwenye beji ya FIFA, Israel Mjuni Nkongo amechaguliwa kuchezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) kati ya wenyeji Zesco FC ya Zambia dhidi ya AS Kaloum ya Guinea.

Katika mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili, Nkongo atasaidiwa na washika kibendera John Kanyenye na Josephat Bulali na mwamuzi wa akiba Waziri Sheha wote kutoka Tanzania, huku Kamisaa wa mchezo akiwa Mayixole Elvin Shishana kutoka nchini Afrika Kusini

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 13,14,15 Machi mwaka huu nchini Zambia.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni