.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 4 Machi 2015

MRADI WA KINYEREZI 1 KUKAMILIKA JUNI MWAKA HUU



Meneja Miradi ya Kinyerezi Mhandisi Simon Jilima amesema kuwa mtambo wa Kinyerezi 1 unaojengwa na kampuni ya Yakobsen Elektro ya Norway unatarajia kukamilika mapema Juni mwaka huu.

Mhandisi Jilima aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanya ziara katika mtambo huo ili kujionea maendeleo ya ujenzi wake. Kamati hiyo imeanza ziara ya kutembelea miradi ya umeme iliyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa madini aina ya tanzanite katika mkoa wa Manyara.

Mhandisi Jilima alisema kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 80 na kufafanua kazi inayofanyika kwa sasa ni kumalizia utandazaji wa nyaya, ufungaji wa mabomba ya maji na gesi pamoja na ujenzi wa barabara za ndani.


Alisema kuwa ofisi kwa ajili ya watumishi pamoja na karakana kwa ajili ya kuhifadhia mitambo imekamilika.

Akielezea gharama za mradi huo Mhandisi Jilima alisema mpaka sasa serikali imelipa kiasi cha Dola za Marekani milioni 167.2 na kuongeza kuwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 15 kinatarajiwa kumaliziwa kabla ya kukamilika kwa mradi.

Akielezea changamoto katika utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Jilima alieleza kuwa awali changamoto kubwa ilikuwa ni ukamilishwaji wa mradi wa bomba la gesi ili waweze kutumia gesi hiyo katika kuzalisha umeme lakini kutokana na kasi ya mradi huo kuwa ya kuridhisha wana imani kuwa gesi itaanza kuzalishwa mapema kabla ya kukamilika kwa mtambo wa Kinyerezi 1

“ Ndugu wajumbe, awali tulikuwa na wasiwasi wa kupatikana kwa gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kupitia mradi wa Kinyerezi 1 kutokana na mradi wa bomba la gesi kuwa na changamoto nyingi, lakini baada ya kuona mradi wa bomba la gesi uko katika hatua nzuri yaani zaidi ya asilimia 90, tunaamini kuwa mara mtambo utapokamilika, gesi itakuwa imekwishaanza kuzalishwa na hapo ndipo tutaanza kuzalisha umeme mara moja,” alieleza Mhandisi Jilima

Akielezea fidia kwa wakazi waliopisha ujenzi wa mradi huo, Mhandisi Jilima alieleza kuwa mradi wa Kinyerezi I ulikwishafanya tahmini pamoja na kulipa fidia kwa wakazi waliopisha ujenzi wa mtambo huo tangu mwaka juzi.

Wakati huohuo wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini walipongeza hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mtambo huo na kuitaka serikali kukamilisha malipo ya kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 15 ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni